1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Nigeria wachochea mashambulizi

Admin.WagnerD14 Januari 2015

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema uchaguzi mkuu ujao nchini Nigeria ni suala linalochangia kuongezeka pakubwa mashambulizi yanayofanywa na kundi la Boko Haram kaskazini mwa Nigeria.

https://p.dw.com/p/1EJpF
Picha: Reinnier Kaze/AFP/Getty Images

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Marie Harf amesema chaguzi za rais na ubunge nchini Nigeria zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 mwezi ujao zinapaswa kuendelea licha ya ghasia zilizoikumba nchi hiyo ambazo Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema zimewalazimu takriban watu 20,000 kutorokea nchi jirani katika siku chache zilizopita.

Harf amesema Marekani inaamini kuwa uchaguzi huo wa Februari umechangia katika kuongezeka katika visa vya mashambulizi kutoka kwa waasi wa Boko Haram.

Mashambulizi ya Boko Haram yaongeza taharuki

Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa kinyang'anyiro kati ya Rais Goodluck Jonathan na mpinzani wake mkuu Muhammadu Buhari. Boko Haram inaaminika kutumia kipindi hiki cha uchaguzi kuchochea hali ya taharuki miongoni mwa raia kama mojawapo ya mikakati yake ya kutanua uasi.

Mwanajeshi akishika doria katika mji wa Baga katika jimbo la Borno
Mwanajeshi akishika doria katika mji wa Baga katika jimbo la BornoPicha: Pius Utomi/AFP/Getty Images

Tume ya uchaguzi nchini Nigeria hapo jana ilisema itaandaa uchaguzi katika majimbo matatu ya kaskazini mwa nchi hiyo ambayo ni ngome ya Boko Haram lakini imeonya kuna matumaini finyu kuwa watu watajitokeza kupiga kura katika eneo hilo.

Waasi wa Boko Haram waliuvamia mji wa Baga mnano tarehe tatu mwezi huu na kuwauwa maelfu ya wakaazi wa mji huo. Wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wameshindwa kuingia mji huo kuthibitisha idadi kamili ya waliouawa huku maiti zikizidi kuoza katika barabara za mji huo.

Umoja wa Afrika umelaani vikali mashambulizi hayo mabaya zaidi kuwahi kufanywa na Boko Haram tangu ianzishe uasi kaskazini mwa Nigeria mwaka 2009.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma amesema ameshtushwa na mauaji ya Baga na miripuko ya mabomu yaliyotokea Potsikum pamoja na kuhusishwa kwa washambuliaji wa kike wa kujitoa muhanga na mtoto wa miaka kumi na kuzitaka nchi za Afrika na jumuiya ya kimataifa kuja pamoja na kukabiliana na kitisho cha Boko Haram.

Wanigeria wakimbilia Chad

Msemaji wa shirika la kushughulikia maslahi ya wakimbizi la umoja wa Mataifa UNHCR William Spindler amewaambia wanahabari kuwa asilimia sitini ya wanigeria wanaotorokea Chad ni wanawake na wasichana na kuongeza watoto 84 ambao hawakuandamana na watu wazima pia wameingia nchini humo.

Msemaji wa shirika la umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu Ravina Shamdasani amewaambia wanahabari mjini Geneva kuwa licha ya kutokuwepo kwa taarifa kamili kuhusu shambulizi la Baga,ni bayana kuwa kulifanyika mauaji ya watu wengi na kwamba wakaazi wengi wa mji huo wamelazimika kuyahama makaazi yao.

Shamdasani amesema kushambuliwa kimakusudi kwa raia kunakiuka sheria za kimataifa na wanatiwa wasiwasi na ripoti kuwa watoto na wazee ni miongoni mwa waathiriwa wa mashambulizi ya Boko Haram.

Tangu waasi wa Boko Haram kuanzisha uasi,kiasi ya watu 135,000 wametoroka kutoka eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kiasi ya wengine 850,000 wameachwa bila makaazi katika eneo hilo.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri:Josephat Charo