1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Nigeria waahirishwa

4 Aprili 2011

Tume ya uchaguzi ya Nigeria imeahirisha uchaguzi wa bunge kwa wiki moja baada ya kushindwa kukamilisha maandalizi kwa wakati uliopangwa.

https://p.dw.com/p/10n3N
2.4.2011 in Lagos. Wähler warten, um ihre Wahlausweise vorzuzeigen. Copyright: DW/Thomas Mösch
Wananchi waliokuwa wakisubiri kupiga kura kabla ya kuaahirishwaPicha: DW/Thomas Mösch

Uamuzi huo unaonekana kuwa aibu kwa taifa linalojaribu kuondokana na historia ya chaguzi za machafuko, huku wapigaji kura wakikasirishwa na kuvunjwa moyo na hatua hiyo.

Wapigaji kura wengi walimiminika vituoni Jumamosi iliyopita katika mji wa Lagos wakiwa na matumaini kwamba uchaguzi wa bunge ungefanyika. Karibu kila mahali mjini humo watu walisubiri kwa utulivu na amani kwenye foleni. Kulitokea purukushani kidogo na polisi huku jeshi likipiga marufuku magari yasipite katika barabara za mji huo. Lakini ghafla mkuu wa tume ya uchaguzi akatangaza kusitisha uchaguzi huo.

"Ili kulinda hadhi ya uchaguzi, tume imechukua uamuzi mgumu lakini unaostahili wa kuahirisha uchaguzi wa bunge hadi Jumatatu Aprili 4.

Jaribio la kufanya uchaguzi wa bunge leo liligonga mwamba pale vyama vya kisiasa vilipolalamika kwamba havina muda wa kutosha kujiandaa. Mkuu wa tume ya uchaguzi, Attahiru Jega ameuahirisha tena uchaguzi wa bunge hadi Aprili tisa, huku ule wa rais ukipangwa kufanyika Aprili 16. Uchaguzi wa magavana utafanyika Aprili 26 mwaka huu.

***Für mögliche Ergänzungen der Karte, wie z.B. andere Sprachen, zusätzliche Orte oder Markierungskreuz, wenden Sie sich bitte an infografik@dw-world.de (-2566), Außerhalb der Bürozeiten an bilder@dw-world.de (-2555).*** DW-Grafik: Per Sander 2011_03_10_Laender_Prio_A_B
Uchaguzi wa Bunge utafanyika tarehe 9 Aprili

Kuahirishwa kwa uchaguzi kumezusha hasira miongoni mwa wapigaji kura. Hata gavana wa Lagos, Babatunde Fashola, alikuwa tayari amepiga kura yake wakati habari zilipomfikia kwamba uchaguzi umeahirishwa. Akasema:

"Ni haraka sana kwa tume ya uchaguzi kupendekeza uchaguzi ufanyike Jumatatu, kama wameshindwa kwa kipindi hiki chote, kwa nini wanafanya haraka? Nadhani wanatakiwa kukutana na vyama vyote vya kisiasa na sioni kwa nini hawawezi kuchukua nafasi sasa kuchukua wiki moja kupanga na kuunganisha na uchaguzi wa Jumamosi ijayo."

Matatizo yalijitokeza wakati majina mengi yalipokosekana katika daftari la kupigia kura. Katika vituo vya kupigia kura katika majimbo mengine ya Nigeria, kulikuwa na taarifa za kuwepo matatizo ya uratibu. Matarajio ya wapigaji kura safari hii ni makubwa, huku wengi wakitarajia kwamba serikali mpya itawaletea maji, umeme na kujenga barabara katika maeneo wanakoishi.

Matumaini kwamba uchaguzi ungeleta mageuzi sasa kwa wapigaji kura wengi yamedidimia kutokana na aibu ya siku ya Jumamosi. Hata hivyo Wanigeria wana fursa ya kubadili siasa za nchi yao Jumamosi ijayo.

Mwandishi: Mösch, Thomas Lagos DW Afrika/Josephat Charo

Mhariri: Abdul-Rahman