Uchaguzi wa mkoa wa Tain yumkini ukaamuwa nani wa kuiongoza Ghana
2 Januari 2009Afisa wa uchaguzi amesema uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa kwa sababu hawakupatiwa nyaraka za mahkama za kusitisha uchaguzi huo kama vile chama tawala cha NPP kilivyosema kuwa zimepatiwa nyaraka hizo.
Marudio hayo ya uchaguzi yalianza kuonekana kama sio ya uhakika hapo jana wakati chama tawala kilipokwenda mahkamani mara mbili kwanza katika jaribio la kuzuwiya kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi na halafu kuzuwiya kufanyika kwa uchaguzi wa Tain.
Kwanza chama hicho cha NPP kilitaka kuzuiliwa kwa tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya Tain hadi hapo madai yake ya kukiukwa kwa taratibu za kura katika ngome kuu za chama hicho yatakapokuwa yamefanyiwa uchunguzi. Lakini mahkama imesema itasikiliza kesi hiyo hapo Jumatatu siku mbili baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
NPP baadae ilirudi mahkamani na ombi jipya la kutaka kucheleweshwa kwa uchaguzi huo kwa hoja kwamba mazingira huko Tain hayafai kwa uchaguzi huru na wa haki. Chama hicho tawala kinasema mahkama ilipitisha hukumu ya kuwaunga mkono lakini mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kwadwo Afari-Gyan amesisitiza kwamba uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa.
Habari pia zinasema kwamba chama cha NPP kimetishia kususia uchaguzi huo.
Katika mji mkuu wa Accra ofisi za kampeni za vyama wiwili vikuu zilikuwa tupu kabisa wakati macho yote na nguvu zote zikiwa zimeelekezwa katika jimbo hiklo la uchaguzi la Tain lilioko magharibi mwa nchi hiyo.
Jimbo hilo la uchaguzi lilishindwa kupiga kura hapo Jumapili kwa sababu ya matatizo katika usambazaji wa makaratasi ya kupigia kura na kwa sababu matokeo rasmi hadi sasa yameshindwa kutowa mshindi wa moja kwa moja na kwa hiyo matokeo ya jimbo hilo moja kwa moja yanaweza kuamuwa nani wa kuingoza Ghana kwa kipindi kijacho cha miaka minne.
Matokeo rasmi kutoka majimbo mengine ya uchaguzi 229 yameonyesha kiongozi wa upinzani John Atta- Mills akiongoza kwa kura chache dhidi ya mgombea wa chama tawala Nana Akufo- Addo.
Leo itakuwa mara ya tatu katika kipindi cha mwezi mmoja kwamba Ghana nchi inayonekana kuwa mfano wa demokrasia kwa Afrika kujaribu kumchagua rais wa kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Waghana kwanza walipiga kura hapo tarehe saba mwezi wa Desemba lakini wagombea walishindwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika kwa ushindi lakini mgombea wa chama tawala Akufo-Addo alikuwa akiongoza.
Usalama umeimarishwa katika jimbo hilo la uchaguzi la Tain ambalo baadhi ya wanaharakati wa kisiasa wanalilinganisha la jimbo la Florida la Marekani hapo mwaka 2000 ambalo ndilo lililotowa maamuzi na ushindi tata kwa muhula wa kwanza wa urais kwa Rais George W. Bush.
Mamia ya wanajeshi na polisi wenye silaha wamemwagwa huko na katika miji mengine ya Tain ukaguzi mkubwa wa usalama umewekwa kwenye barabara kuelekea kwenye mji mkuu wa wilaya ya Tain wa Nsawkaw ambapo magari yamekuwa yakipekuliwa kutafuta silaha zilizofichwa.
Kwa mujibu wa repoti za vyombo vya habari kutoka mkoa huo wanaharakati wamekuwa wakifanya kampeni ya nyumba hadi nyumba ambapo timu ya upinzani imekuwa ikiongozwa na kiongozi wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings.
Chama cha upinzani cha MDC kilishinda uchaguzi huko Tain katika duru ya kwanza na kinashikilia kiti cha ubunge cha jimbo hilo la uchaguzi.
Uchaguzi huo ambao wachambuzi wa mambo wanasema ni mchuano mkubwa kabisa katika historia ya Afrika umezusha hali ya mvutano kati ya vyama hivyo vikuu viwili juu ya kwamba waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wamesema uchaguzi huo hadi sasa umekuwa wa utulivu na wa wazi.