1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Nini kinatokea siku ya uchaguzi Marekani na baada yake?

5 Novemba 2024

Nchini Marekani vituo vya kupigia kura vimefunguliwa. Wananchi wenye haki ya kupiga kura wataamua kama watampeleka Kamala Harris au Donald Trump katika Ikulu. Uchaguzi unafanyikaje na mchakato wa kuhesabu kura unaendaje?

https://p.dw.com/p/4mcHm
Uchaguzi wa Marekani 2024 | Wapigakura wa Virginia wakipigia kura zao
Wamarekani wanachagua kati ya Donald Trump na Kamala HarrisPicha: Samuel Corum/Sipa USA/picture alliance

Watu takriban milioni 244 wenye umri wa miaka 18 na zaidi ndiyo wana haki ya kupiga kura. Hata hivyo, katika baadhi ya majimbo ya Marekani, wale waliopatikana na hatia ya makosa makubwa ya jinai hawaruhusiwi kupiga kura.

Kando na rais, wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Seneti pia wanachaguliwa. Jumla ya viti 469 vinagombaniwa, 34 katika Seneti na 435 katika Bunge la Wawakilishi.

Wapiga kura wanaweza kupiga kura kwa njia tatu: kupiga kura mapema, kwa njia ya posta, au kufika kwenye vituo vya kupigia kura siku ya uchaguzi. Majimbo 47 yalianza upigaji kura wa mapema mwezi Septemba. Kwa mfano, Virginia ilianza Septemba 20, ikifuatiwa na California, Texas, na Florida mwezi Oktoba.

Majimbo ya maamuzi yanayoitwa "swing states" yana nafasi muhimu kwenye uchaguzi huu. Haya ni majimbo ambayo hayaegemei moja kwa moja kwa cham cha Democratic au Republican na yanaweza kubadilisha matokeo.

Uchaguzi wa Marekani 2024 | Kamala Harris mgombea wa Democratic
Mgombea wa chama cha Democratic Kamala HarrisPicha: John Moore/Getty Images

Mwaka huu, majimbo muhimu ni Arizona, Georgia, Michigan, Nevada, North Carolina, Pennsylvania, na Wisconsin. Majimbo haya yanaweza kuamua mshindi wa uchaguzi.

Soma pia: Wafahamu wagombea urais Marekani na sera zao

Kwa kuwa Marekani ina majira sita tofauti ya muda, vituo vya kupigia kura vinafunguliwa na kufungwa kwa nyakati tofauti. Vituo vingi hufungwa kati ya saa moja na saa mbili usiku kwa muda wa maeneo husika. Hata hivyo, kwa majimbo kama New York, vituo hufungwa saa tatu usiku.

Zoezi la kuhesabu kura hadi kuapishwa rais

Mara vituo vya kupigia kura vinapofungwa, zoezi la kuhesabu kura huanza mara moja katika katika vituo vyao kote nchini humo. Kura za posta hufanyiwa utaratibu tofauti kwa majimbo mbalimbali. Katika baadhi ya majimbo, haziwezi kuhesabiwa hadi siku ya uchaguzi, lakini kwa mengine, zinaweza kuanza kuhesabiwa mapema.

Rais atakayeshinda atahitaji kura 270 kati ya 538 za wajumbe wa uchaguzi. Marekani inatumia mfumo wa wajumbe - unaoitwa Electoral College, ambapo mshindi wa kura za wananchi si lazima apate kura nyingi zaidi kitaifa bali apate wajumbe wa kutosha kutoka majimbo.

Soma pia: Putin asema Marekani itaamua yenyewe uhusiano baina yao

Hii ilitokea mwaka 2016, ambapo Hillary Clinton alipata kura nyingi lakini Trump akapata wajumbe wengi zaidi.

Uchaguzi wa Marekani 2024 | Donald Trump mjini Wisconsin
Donald Trump anatupa karata yake kwa mara ya tatu, baada ya kushindwa na Joe Biden katika jaribio lake la kutasaka muhula wa pili mwaka 2020.Picha: CHIP SOMODEVILLA /AFP/Getty Images

Ikiwa wagombea wawili watapata kura sawa, Bunge la Wawakilishi litachagua rais, huku kila jimbo likipata kura moja pekee.

Kwa kawaida, matokeo ya mwisho hutangazwa siku hiyo. Hata hivyo, ikiwa kuna pingamizi kwenye matokeo ya majimbo, sharti litatuliwe kufikia Desemba 11.

Wajumbe hukutana rasmi Desemba 17 ili kumpiga kura rais na makamu wake, na mnamo Januari 6, Kongresi itahesabu kura za wajumbe na kutangaza mshindi rasmi. Rais mpya ataapishwa Januari 20 mwaka 2025.

Mwandishi: Prange de Oliveira, Astrid