1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge Madagascar waahirishwa

10 Januari 2011

Uamuzi huo umefikiwa na wanasiasa nchini humo ili kuruhusu muda zaidi wa kufanya maandalizi.

https://p.dw.com/p/zvxl
Kiongozi wa Madagascar, Andry Rajoelina.Picha: picture-alliance/ landov

Wanasiasa nchini Madagascar wamekubaliana kuahirisha uchaguzi wa bunge uliokuwa ufanyike Machi 16 mwaka huu, ili kuruhusu muda zaidi kufanya maandalizi. Kwa mujibu wa gazeti la L´Express de Madagascar, uamuzi huo ulipitishwa kwenye mkutano kati ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Camille Vital na wajumbe wa vyama vya kisiasa nchini humo.

Kugundulika kwa mapungufu kwenye orodha ya majina ya wapigaji kura wakati wa kura ya maoni kuhusu katiba mwezi Novemba mwaka jana, ni sababu nyengine iliyotolewa kwa kuahirishwa uchaguzi huo. Suala lengine lililozingatiwa ni msimu wa mvua katikati ya mwezi Aprili, ambazo husababisha barabara zisipitike na kuyafanya maeneo mengi ya Madagascar kutoweza kufikiwa.

Chaguzi za manispaa zilizopangwa kufanyika Desemba 20 mwaka jana, ziliahirishwa pia kwa sababu za uratibu, bila tarehe mpya kutangazwa. Meya wa zamani wa mji mkuu Antananarivo, Andry Rajoelina, alimuondoa madarakani aliyekuwa rais wa Madagascar, Marc Ravalomanana, kwenye mapinduzi ya kijeshi mnamo mwezi Machi 2009 na kujiapisha kama rais wa mpito.