1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge la Ulaya waanza Uholanzi na Uingereza

John Juma Mhariri: Josephat Charo
23 Mei 2019

Jumla ya wapiga kura milioni 400 wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo katika nchi 28 wanachama wa umoja huo. Jumla ya wabunge au wawakilishi 751 kuchaguliwa.

https://p.dw.com/p/3IwUE
Deutschland | Europawahlen 2014
Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Uchaguzi wa bunge la Ulaya umeanza leo. Uholanzi na Uingereza ndizo nchi ambazo wapigakura wao wanashiriki leo kuwachagua wawakilishi wao katika bunge hilo. Jumla ya nchi 28 wanachama zinatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo utakaodumu kwa siku nne. 

Nchi mbili pekee ndizo zinafanya uchaguzi wa bunge la Ulaya kwa siku ya leo Alhamisi, zikiwa ni Uholanzi na Uingereza.

Nchini Uholanzi, vituo vya upigaji kura vilifunguliwa mapema na nusu saa baadaye zoezi hilo pia likaanza Uingereza, nchi ambayo inakabiliwa na msukosuko wa kupata muafaka wa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Jumla ya wapiga kura milioni 400 wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo katika nchi 28 wanachama wa umoja huo. Jumla ya wabunge au wawakilishi 751 wanatarajiwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi huo unaotajwa kuwa miongoni mwa chaguzi za kidemokrasia zaidi ulimwenguni.

Nchini Uingereza, kura ya maoni inaonyesha kuwa chama kipya cha Brexit kitapata ushindi wa kati ya asilimia 30-40 za kura dhidi ya vyama viwili vikuu, kinachotawala cha kihafidhina ‘Conservatives' na kile cha upinzani ‘Labour.'

Wafuasi wa zamani wa chama cha waziri Mkuu Theresa May, wanatarajiwa kukiunga mkono chama cha Brexit, kutokana na mkwamo uliopo wa Uingereza kushindwa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na kusababisha wao kushiriki uchaguzi huo.

Nchini Uingereza, wachambuzi wa siasa wanabashiri kuwa suala tete la Brexit litakuwa na ushawishi mkubwa.
Nchini Uingereza, wachambuzi wa siasa wanabashiri kuwa suala tete la Brexit litakuwa na ushawishi mkubwa.Picha: picture-alliance/dpa/ANP/B. Maat

Inatarajiwa pia kuwa waliberali wanaopinga Brexit na ambao wanataka kuwe na kura ya maoni ya pili kuhusu Brexit watajitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi huo.

Wachambuzi wa siasa wanabashiri kuwa suala tete la Brexit litakuwa na ushawishi.

Nchini Uholanzi, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia ‘Forum for Democracy (FvD), kinatarajiwa kuwa na ushindani mkali na chama cha waziri mkuu Mark Rutte Conservative Liberal (VVD).

Uchaguzi huo pia unaleta hali ya kupimana nguvu kati ya wale wanaotaka Umoja wa Ulaya uimarishwe dhidi ya wale wanaoendeleza siasa za kizalendo na wanataka serikali za nchi zao kuwa na mamlaka zaidi kujiimarisha kivyao. Ohan Van Overtveld anayegombea ubunge kutoka Ubelgiji anazungumzia suala hilo:

"Hicho ndicho tunachoona kwenye uchaguzi kwamba vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia hakika vinashinda viti vingi, kura nyingi na hilo si jambo zuri kwa Ulaya na kwa raia."

Kuna hofu kuwa huenda vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vitabadili hali katika bunge la Ulaya.
Kuna hofu kuwa huenda vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vitabadili hali katika bunge la Ulaya.Picha: Reuters/P. van de Wouw

Wengi wanahofia kuwa hali itabadilika katika bunge la Ulaya ambalo kwa miaka 40 limekuwa na vyama vingi vya kati kulia na kati kushoto, kufuatia vyama vya kizalendo ambavyo vimejipenyeza katika mataifa ya Italia, Ufaransa, Hungary na Ujerumani.

Bunge jipya litakuwa muhimu katika kuwateua wakurugenzi wapya wa Umoja wa Ulaya na kamisheni ya Umoja wa Ulaya kabla ya kuanza kazi yake ya kuidhinisha miradi mipya ya umoja huo kama vile kupitisha bajeti.

Mataifa ya Ireland na Jamhuri ya Czech yanatarajiwa kufanya uchaguzi wao kesho Ijumaa. Latvia, Malta na Slovakia zitashiriki siku ya Jumamosi, kisha mataifa 21 yaliyosalia ya Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani yatashiriki uchaguzi huo Jumapili.

Matokeo rasmi hayatatolewa hadi baada ya uchaguzi kumalizika Jumapili usiku.

Vyanzo: APE, DPAE