1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge la Mkoa wa Hamburg

Miraji Othman22 Februari 2008

Kesho, jumapili, wananchi wa mji wa Hamburg watachagua bunge la mkoa wao, ikiwa uchaguzi watatu wa kimkoa mnamo mwaka huu.

https://p.dw.com/p/DBxv
Watetezi wa Umeya-mkuu wa Hamburg, Ole von Beust wa CDU (kushoto)na Michael Naumann wa SPD (kulia)Picha: AP

Uchaguzi huu pia unatazamiwa utakuwa wa kusisimua, kwani, kama vile ilivotokea wiki chache zilizopita katika mkoa wa Hessen, huenda tena mara hii chama ambacho kilikuwa hakitiliwi maanani sana upande wa Magharibi wa Ujerumani, Chama cha Kushoto, kikaingia bungeni. Kutokana na hali hiyo, uwingi wa vyama vikubwa vya Christian Democratic, CDU, na Social Democratic, SPD, utabadilika, kihesabu. Ndio maana vyama hivyo viwili vinawania kuwang'ang'ania wapigaji kura wao. Zaidi anayo Othman Miraji◄

"Mimi nahisi serekali ya mkoa ya chama cha CDU imefanya makosa mengi."

"Sifichi kwamba mimi namthamini Bwana von Beust na ningependa kuona kwamba yeye anaendelea kuwa meya mkuu wa jiji la Hamburg."

"Chama cha SPD kilikuwa miaka 30 madarakani, Kimefanya nini? Hakijafanya chochote."

Kutakuwa na msisimko mkubwa katika mji wa Hamburg, kwani haitarajiwi kwamba kuna chama kitakachopata wingi ulio wazi katika uchaguzi huo ambapo wakaazi miilioni 1.3 watakuwa na haki ya kupiga kura.Kwa wiki na miezi kadhaa sasa kumefanywa kampeni za uchaguzi katika mji huo; wanasiasa , bila ya kuchoka, wamekuwa wakisimama masokoni, madukani, mabarabarani na kwenye mikutano ya hadhara ili kuwashawishi wananchi wakubaliane na fikra zao. Na hasa, meya mkuu wa mji huo anayetokea Chama cha CDU, Ole von Beust, na ambaye katika miaka minne iliopita ametawala akiwa na wingi ulio wazi bungeni.

"Sisi tunaongoza katika kuunda nafasi mpya za kazi, hivyo , kwa pamoja, tunaweza kuwa na fahari. La pili tumefanya jitihada kubwa pamoja na raia kuitengeneza vizuri bajeti yetu, hivyo kutochukuwa madeni.Jambo la tatu ni kwamba kutokana na uchumi kuwa imara na kuweko nafasi za kazi pamoja na bajeti isiokuwa na nakisi, sasa tunaweza kugharimia yale mambo muhimu katika mji, shule za msingi, miradi ya kitamaduni na mengine na mengine.. Lakini huo ndio mpangilio. Kwanza kuchuma halafu kugawa kile kilichopatikana."

Mji unakuwa na pia umaskini, hivyo ndivyo anavosema mtetezi wa kiti cha meya-mkuu kutoka Chama cha Social Democratic, SPD, Michael Naumann. Mwandishi huyo wa habari na hivi sasa akiwa likizoni kama mchapishaji wa jarida la kila wiki la DIE ZEIT, amepanda haraka kisiasa. Chama cha SPD kinachuana vikali na chama cha CDU huko Hamburg.

"Hamburg lazima ikuwe kwa pamoja. Mji wa Hamburg maisha ulikuwa una nguvu, pale wizani wa usawa wa kijamii unapokuwa barabara. Sisi wanachama wa Social Democratic tunasimama kupigania usawa wa kijamii. Hiyo ina maana kwamba neema ya uchumi katika Hamburg mwishowe raia lazima waihisi katika mifuko yao."

Chama cha Social Democratic kingependa kuunda serekali ya mseto na Chama cha Kijani, Lakini wakati wa kampeni, kumezungumziwa pia uwezekano wa kuundwa serekali ya mseto kati ya Chama cha Christian Democratic, CDU, na kile cha Kijani. Raia wa Hamburg wamechanganyikiwa, hawajuwi waamuwe vipi.

Lakini angalau vyama viwili ni hakika vitaingia bungeni, navyo ni CDU na SPD. Chama cha shoto, ambacho kinaingia kwa mara ya kwanza katika mchuano huu wa Hamburg, kutokana uchunguzi wa maoni, kinatarajiwa kupata asilimia tisa ya kura. Marcus Donath wa Chama cha Shoto analiangalia hivi jukumu lao litakavokuwa:

"Nafikiri kazi ya Chama cha Shoto itakuwa pia kukiweka kidole katika jaraha la jamii na kuonesha wapi matatizo na ukosefu wa haki ulipo. Na pia mara kadhaa tutaamua kwenda kwa wananchi na kujiarifu juu ya makosa yanayofanyika. Sisi, kwa vyovyote, hatutashiriki katika mchezo wa uchu wa madaraka, mchezo wa kutaka tu kukamata nyadhifa."

Hivyo kinabaki chama cha kiliberali cha Free Democratic, FDP. Katika uchaguzi uliopita, chama hicho kilipata asilimia 2.8 tu ya kura. Hivi sasa inakisiwa kwamba kitapata asilimia tano, hivyo kutaraji kuwakilishwa bungeni.