1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa awali Marekani kuanza Iowa

1 Februari 2016

Wagombea wanaowania uteuzi wa vyama vya Republican na Democratic wamewahimiza wapiga kura wa jimbo la Iowa katika dakika za lala salama kabla kufanyika uchaguzi wa kwanza wa awali leo. (01.02.2016)

https://p.dw.com/p/1Hn3A
DW Reihe What America do you want Bernie Sanders' America
Picha: DW/R. Walker

Kufikia leo jioni wagombea wanaowania uteuzi wa vyama vya Republican na Democratic katika uchaguzi wa urais wa Marekani mwaka 2016 watajua kama muda wao, jitihada zao na fedha walizotumia katika kampeni zao zimefaulu kwa kuwavutia wapigaji kura wengi, jambo litakalozipa msukumo kampeni zao wakati kinyang'anyiro kitakapohamia jimbo la New Hampshire.

Mgombea wa chama cha Republican Donald Trump na mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton wanaongoza katika kura za maoni lakini hawana idadi kubwa ya kutosha kuwahakikishia ushindi wa wazi katika uchaguzi wa awali wa vyama vyao hivi leo.

Je Marco Rubio wa Republican pengine ataungwa mkono na kukifanya kinyang'anyiro cha Warepulican kuwa cha watu watatu, yaani Donald Trump na mhafidhina Ted Cruz? Na je msoshalisti wa chama cha Democratic aliyejitangaza mwenyewe, Bernie Sanders, atafaulu kuyageuza mapinduzi yake ya kisiasa kuwa kura za kutosha kumpiku Hillary Clinton anayejaribu kushinda uteuzi wa chama kwa mara ya pili?

USA Wahlkampf Demokraten Präsidentschaftskandidaten TV-Debatte
Hillary Clinton (kushoto) na Bernie SandersPicha: Reuters/R. Hill

Kampeni za wagombea wote hawa zinakabiliwa na mtihani kwa mara ya kwanza - watu wazuri wa Iowa.

Umuhimu wa dini na mafuta

Kabla kujiondoa katika mchuano wa kuwania uteuzi wa chama cha Republican, seneta wa jimbo la South Carolina Lindsey Graham alijifunza mambo mawili muhimu alipokuwa akifanya kampeni Iowa: Unahitaji kumpenda Yesu na mafuta yanayotokana na mimea ya ethanol. Dini ina jukumu muhimu katika chaguzi za awali za chama cha Republican katika majimbo ya katikati magharibi mwa Marekani. Mwaka 2012 karibu asilimia 60 walioshiriki walijitambulisha kama wakristo wa makanisa ya kiinjili.

Iowa ni jimbo la kwanza kuwapigia kura wagombea urais wa Marekani. Anayeshinda hupata nguvu katika kampeni zake za urais. Hii pengine ndio sababu kwa nini bilionea Donald Trump, ambaye si maarufu kwa imani yake ya kidini, alitoa hotuba katika chuo kikuu kikubwa duniani cha kanisa la kiinjili, Liberty, wiki mbili kabla uchaguzi wa Iowa.

Hotuba yake katika chuo hicho ilimfanya kuungwa mkono na mkuu cha chuo hicho, Jerry Falwell Jr, ambaye baba yake alikuwa mmojawapo wa wahubiri waliokuwa na ushawishi mkubwa katika historia ya hivi karibuni ya Marekani. Haijabainika wazi kama hatua hii itampiga jeki Trump jimboni Iowa.

USA Wahlkampf Donald Trump Soloauftritt Iowa
Donald TrumpPicha: Reuters/A. P. Bernstein

Kama dini ni suala kubwa la siasa Iowa, basi hata mafuta ya ethanol nayo pia. Jimbo hilo linalazalisha geleni bilioni 3.9 za mafuta haya yanayotokana na mimea, ikiwa ni asilimia 27 ya uzalishaji jumla wa Marekani. Huku Trump akiwa amepata tabu kupata dini, mpinzani wake mkuu, seneta wa jimbo la Texas Ted Cruz, ana shida ya ethanol. Trump na Cruz wanakabana koo katika kura za maoni.

Sanders dhidi ya Clinton

Kwa upande wa chama cha Democratic, ujumbe wa Bernie Sanders kuwafuatilia mabilionea na kupigania usawa wa mishahara umepokewa vyema na wapiga kura. Lakini wengi wao wanathamini sana uzoefu mpana wa Hillary Clinton kama mke wa rais Bill Clinton, seneta wa jimbo la New York na waziri wa mambo ya nje wakati wa utawala wa rais wa sasa Barack Obama.

Clinton pia amejiwasilisha kama mrithi wa Obama ambaye amebaki kuwa maarufu miongoni mwa wafuasi wa chama cha Democratic, kama sio miongoni mwa Wamarekani wengi kwa ujumla.

Mwandishi:Spencer Kimball

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Iddi Sessanga