Uchaguzi Tanzania: Changamoto za upigaji kura Arusha Mjini
28 Oktoba 2020Hali ni ya utulivu katika jiji la Arusha, hakuna pirika pirika nyingi zinazoshuhudiwa kama siku zingine. Leo ikiwa ni siku ya mapumziko biashara nyingi zimefungwa na idadi ya watu wanaotumia usafiri wa umma pia ni ndogo sana.
Mada kubwa inayojadiliwa katika magari ya umma ni zoezi la upigaji kura. Katika eneo la Kaloleni miongoni mwa vituo 910 vya kupigia kura vilivyopo katika jiji la Arusha wapiga kura wameelezea kuchelewa kuanza kwa zoezi hilo kwa kile kilichoelezwa kwamba karatasi za kupigia kura zilichelewa kufika.
Fatuma, mmoja wa wapiga kura katika eneo hilo, amesema kuwa hali ni shwari katika eneo hilo lakini makaratasi ya kura ndiyo yaliocheleweshwa.
Katika kituo kingine cha Ilboru shule ya msingi jimbo la uchaguzi la Arumeru magharibi baadhi ya watu ambao tayari wamekwisha piga kura wameelezea kushangazwa na hali ya kutokuwa na mawakala katika vituo hivyo huku wengine wakirudi nyumbani bila kupiga kura baada ya kukosa majina yao katika vituo.
Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika kituo cha shule ya msingi Ilboru namba moja Rozila Clement, anakiri kuwepo kwa changamoto ya kutokuwa na mawakala ya baadhi ya vyama wakati wa kuanza kwa zoezi hilo. Hakuna tukio la uvunjifu wa amani ambalo limejitokeza kufikia sasa.