Uchaguzi Tanzania: CCM yapata viti vingi, upinzani wapoteza
29 Oktoba 2020Wanasiasa wa upinzani wanasema zoezi la uchaguzi huo wa jana lilighubikwa na kasoro
Utaratibu wa kuhesabu kura unaendelea Tanzania Baraza na Visiwani Zanzibar, baada ya wagombea wa upinzani kulalamika hapo jana kuwa mawakala wao walitupwa nje ya vyumba vya uchaguzi, na kuripoti kugunduliwa kwa masanduku yaliyojazwa kura bandia.
Kulingana na matokeo ya awali ambayo yanatangazwa kupitia kituo cha taifa cha televisheni, chama kikuu cha upinzani, CHADEMA kimepoteza viti muhimu vya ubunge, kikiwemo cha jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro kilichokuwa kikikaliwa na mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Mbowe amesema kilichotokea jana hakiwezi kuitwa uchaguzi, na kuongeza kuwa kulikuwepo vurugu na visa vingi vya kuchukiza katika maeneo yote ya Tanzania.
Huko visiwani Zanzibar, afisa mmoja wa chama kikuu cha upinzani upande huo, Muhene Said Rashid aliwaonyesha waandishi wa habari rundo la karatasi za kupigia kura zilizotiwa mhuri na alama mbele ya jina la Rais Magufuli, ambazo alidai zimekamatwa mikononi mwa wakereketwa wa chama cha mapinduzi.
Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Semistocles Kaijage amesema tume haijapokea malalamiko yoyote kuhusu masanduku hayo ya kura za kughushi, na kuwataka Watanzania kuyachukulia kama uvumi.
Jimbo jingine muhimu lililobadili kambi ni la Mbeya mjini, ambalo limechukuliwa na mgombea wa CCM Tulia Ackson, aliyemshinda Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, ambaye amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 10 iliyopita.
Mkurugenzi wa uchaguzi katika Tume ya taifa ya uchaguzi, Wilson Charles Mahera amesema tume hiyo imeanza kupokea report za uchaguzi wa rais, na kwamba baada ya kuzihakiki wataanza kuzichapisha muda wowote.
Rais wa sasa John Pombe Magufuli ambaye anawania muhula wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, anapambana na Tundu Lissu wa CHADEMA, ingawa wapo wagombea wengine zaidi ya kumi ambao wanachukuliwa kama wasindikizaji.
Magufuli anayetimiza miaka 61 leo, alichaguliwa mwaka 2015 kama kiongozi wa watu aliyelivalia njuga tatizo la rushwa, lakini anakosolewa sana kwa kuwa na mienendo ya kiimla, kuukandamiza upinzani na kuukaba koo uhuru wa watu kujieleza.
Tundu Lissu mwenye umri wa miaka 52 alirejea nchini Tanzania mwezi Julai baada ya kuishi nje ya nchi kwa miaka mitatu, kufuatia shambulizi la risasi ambalo anasema lilikuwa na lengo la kumtoa uhai. Kurudi kwake kulionekana kuipa nguvu mpya kambi ya upinzani.
Kwa upande wa Zanzibar, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya visiwa hivyo vyemnye mamlaka ya ndani Thabit Idarous Faina, amearifu kuwa huko pia zoezi la kuhesabu kura linaendelea, na kwamba mshindi wa kinyang'anyiro cha urais atajulikana katika muda wa saa 24 zijazo.
Mgombea wa chama cha ACT-Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad amekituhumu chama tawala CCM kujaribu kuiba kila kura inayopigwa tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi, hoja ambayo inaafikiwa na waangalizi wa kimataifa.
Vipo viti vya bunge 264 vinavyogombaniwa katika uchaguzi huu, ambao unawashirikisha wapiga kura wapatao milioni 29, na ambao kwa sehemu kubwa haukuwa na waangalizi kutoka nje ya nchi.