Uchaguzi Poland
21 Juni 2010Bronislaw Komorowski, ambaye ni Rais wa muda na spika wa bunge la Poland, ameshinda kwa asilimia 41 dhidi ya asilimia 37 ya kura zote zilizopigwa aliyopata mpinzani wake mkubwa Jaroslaw Kaczynski, ambaye ni pacha wa Rais aliyefariki, Lech Kaczynski.
Matokeo hayo ya awali ni kwa mujibu wa asilimia 94 ya kura zote ambazo zimeshahesabiwa hadi sasa.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa baadaye leo.
Licha ya kuongoza katika matokeo hayo, Bwana Komorowski ameshindwa kupata asilimia 50 ya kuweza kutangazwa mshindi wa moja kwa moja.
Uchaguzi huo wa jana umefanyika kuweza kumpata mrithi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Lech Kaczynski, ambaye alifariki Aprili 10, pamoja na mkewe na wanasiasa na watu wengine maarufu wa nchi hiyo wapatao 95, kwa ajali ya ndege iliyotokea magharibbi mwa Urusi.
Katika kura ya maoni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Komorowski alikuwa akiongoza kwa karibu asilimia 50.
Duru ya pili ya uchaguzi inatarajiwa kufanyika Julai 4, kwa viongozi hao wawili kuchuana bila ya wagombea wengine wanane walioshiriki katika uchaguzi wa jana.
Akizungumza jana mara baada ya zoezi la upigaji kura kumalizika, mgombea wa nafasi ya Urais na Rais wa muda wa nchi hiyo Bronislaw Komorowski amewahamasisha wafuasi wake kujiandaa kwa duru ya pili ya uchaguzi Julai 4.
Rais huyo wa muda wa Poland aliwapongeza pia wagombea wengine wanane, waliokuwa wakiwania nafasi hiyo, hususan chama kinachofuata mrengo wa shoto kwa kupata matokeo yaliyoshangaza.
Licha ya kutolewa kwa matokeo hayo, mgombea wa Urais Jaroslaw Kaczynski amesema uchaguzi bado haujaisha na kwamba wanahitaji kushinda na watashinda.
Katika kampeni zake za uchaguzi alisema kwamba chama chake kinahitaji kushinda kwa ajili ya kuleta hali nzuri kwa Poland.
Asilimia 55 ya Wapoland ndio waliopiga kura katika uchaguzi wa jana jumapili, kuweza kupatikana mrithi atakayechukua nafasi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Lech Kaczynski aliyefariki kwa ajali ya ndege Aprili mwaka huu nchini Urusi.
Idadi ya watu wenye uwezo wa kupiga kura nchinin Poland ni milioni 30.5 na vituo vya kupigia kura 25,000 nchi nzima.
Katika hatua nyingine, wawekezaji na masoko ya hisa nchini humo yanahitaji Bwana Komorowski ashinde kwa vile anatarajiwa kufanya kazi kwa ukaribu na maelewano na serikali ya Waziri Mkuu Donald Tusk, katika kukabiliana na nakisi kubwa ya bajeti ya serikali.
Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, Reuters)
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed