Uchaguzi Nigeria ni mfano mzuri kwa Afrika
19 Aprili 2011Waangalizi kutoka Nigeria na wale wa kimataifa wameuelezea uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika siku ya Jumamosi kuwa moja kati ya chaguzi zilizotayarishwa vizuri zaidi katika muongo huu nchini humo. Kama ilivyotarajiwa rais Goodluck Jonathan ndie mshindi wa uchaguzi huo. Wapinzani wake walishindwa kabla ya uchaguzi huo kujiunga pamoja. Na sasa wanapaswa kukiri kushindwa kwao.
Uchaguzi ni mapambano ya kufa na kupona. Hali hii imekuwa ikionekana katika siasa za Nigeria miongo kadha iliyopita. Ndio sababu kumekuwa na hali ya udanganyifu kila mara katika chaguzi, hususan kwa wale walioko madarakani. Ndio sababu kunatokea ghasia na machafuko, iwapo kunajionyesha hali ya kushindwa. Hali mbaya zaidi ilijitokeza mika minne iliyopita, wakati wa utawala wa rais Olusegun Obasanjo. Aliongoza uchaguzi uliomwingiza madarakani mtu aliyechukua nafasi yake Umaru Musa Yar'adua mwaka 2007 ambapo kulikuwa na hali ya wazi ya udanganyifu, ambapo yeye binafsi aliahidi kuwa hali kama hiyo kitu haitarudiwa tena. Yar'adua hakuweza kuishi kwa muda mrefu hata hivyo, kuweza kutimiza ahadi hiyo.
Lakini mrithi wake Goodluck Jonathan ameifanya ahadi hii kuwa yake. Baada ya uchaguzi wa bunge hapo Aprili 9 na kisha uchaguzi wa rais siku ya Jumamosi, tunaweza kusema , kwamba ameweza kufanikisha. Haijawahi kutokea Nigeria kufanya uchaguzi uliotayarishwa vizuri na wa wazi. Matokeo katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo yanaonyesha kuwa chama tawala PDP kimepoteza kura nyingi kuliko ilivyokuwa miaka minne iliyopita. Upande wa kaskazini mpinzani mkuu wa Jonathan , Muhammadu Buhari amepata kura nyingi.
Ni kitu cha kawaida kwamba mtu anashangaa kuona matokeo ya kura kutoka katika eneo anakotoka Jonathan la Niger Delta na majimbo jirani , ambapo rais angepata hadi asilimia 99. Mtu hawezi kuamini . Kwa hapa tume ya uchaguzi na serikali za majimbo zinapaswa kujibu maswali kadha. Hata kama ni jambo la kawaida kuwa Jonathan angepata asilimia 80 hadi 90 upande wa kusini na kusini mashariki, kwa matokeo jumla hali hiyo isingebadilika.
Upinzani kutoka chama cha CPC cha Buhari na kile ambacho kimekuwa na matokeo mazuri upande wa kusini magharibi cha ACN vinapaswa vyenyewe kujilaumu, kwamba havikuweza kupata ushindi dhidi ya PDP. Hakuna mtu aliyeweza kuamini , kwamba mgombea pekee wa upinzani anaweza kukishinda chama tawala.
Hawakuweza ama hawakutaka kukubaliana . Aliyeweza kuchekelea hilo hata hivyo ni chama tawala cha PDP. Buhari anapaswa kutambua hilo na kukubali matokeo. Anapaswa hivi sasa kupinga hadharani machafuko na ghasia na kuamua kukubali demokrasia.
Kwa upande wa chama cha PDP , pia kinapaswa kujifunza kutokana na uchaguzi huu. Bila sababu yoyote kimevunja makubaliano, ambapo katika uchaguzi huu mwakilishi wa Waislamu wa upande wa kaskazini angepaswa kuwamo. Kwa hiyo Jonathan na chama chake wanawajibika , kutokana na hali ya hisia za kidini zinazojitokeza katika mjadala wa kisiasa na kutokea hali ya ghasia hivi sasa.
Mwandishi : Mösch , Thomas / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman