Uchaguzi nchini Afghanistan
17 Agosti 2009Matangazo
Rais Hamid Karzai na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa urais
nchini Afghanistan leo wanafanya kampeni zao za mwisho kabla ya
uchaguzi wa Alhamisi wiki hii. Hata hivyo tishio la mashambulizi na
ushawishi wa viongozi wa makundi kadhaa ya wapiganaji inatilia
shaka matokeo ya uchaguzi huo wa pili nchini Afghanistan.
Kiongozi wa zamani wa kundi la wapiganaji la Uzbek, generali Abdul
Rashid Dostum alirejea nchini Afghanistan jana kutoka uhamishoni
nchini Uturuki katika kile kinachoonekana kuwashawishi wafuasi
wake kumuunga mkono Rais Hamid Karzai ili apate idadi kubwa ya
kura kuzima uwezekano wa kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.
Kura za maoni zinaonyesha Karzai anaongoza kwa umaarufu, kwa
kiasi cha asili mia 45 na iwapo hatopata asili mia 50 itabidi aingie
tena debeni katika duru ya pili, na mpinzani wake mkuu Abdullah
Abdullah ambaye alikuwa waziri wake wa zamani wa nchi za nje.
Kuzuka kwa mashambulizi pia kunatishia kumharibia Karzai ushindi
wa duru ya kwanza. Wapiganaji wa Kitaliban wameapa kuvuruga
uchaguzi huo, na hili huenda likasababisha idadi ndogo ya watu
kujitokeza kupiga kura hasa katika maeneo yanayokaliwa na kabila la
Pashtun wanaomuunga mkono kwa dhati Hamid Karzai.
Hapo siku ya Jumamosi Wataliban walikiri kuwa ndio waliotekeleza
shambulizi kubwa la bomu katikati mwa mji mkuu Kabul. Wafghani
saba waliuawa na raia wengine 90 kujeruhiwa.
Wanajeshi 30,000 zaidi wa Marekani
wamepelekwa nchini Afghanistan, na kuongeza idadi ya wanajeshi wa
nchi za Magharibi nchini humo kufikia 100,000 kwa mara ya kwanza.
Walid Karzai kakaake Rais Hamid Karzai anasema wamejaribu
kuzungumza na viongozi wa Kitaliban wasichafue uchaguzi.
Vikosi vya kijeshi cha Marekani na Uingereza vimefanya operesheni
kali na hii imesababisha vifo vya wanajeshi wengi zaidi, tangu vita
hivyi vilipoanza miaka minane iliyopita.
Na wakati hayo yaliendelea huko Uingereza waziri mkuu wa nchi hiyo
Gordon Brown anakabiliwa na wakati mgumu kutokana na
kuongezeka kwa vifo vya wanajeshi wa Uingereza nchini
Afghanistan. Jana wanajeshi wengine wanne waliuawa na kufikisha
idadi ya wanajeshi wa Uingereza waliouawa nchini Afghanistan
kufikia 204.
Ingawa Gordon Brown amesisitiza mchango wa Uingereza
Afghanistan ni muhimu- kura za maoni nchini humo zinaonyesha
Wangereza wengi wanasema serikali yao imelemewa nchini
Afghanistan.
Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE
Mhariri: Aboubakary Liongo
Matangazo