Uchaguzi mkuu Zimbabwe mwishoni mwa juma
26 Machi 2008Hali ya kisiasa nchini Zimbabwe inazidi kuwa ya wasiwasi kufuatia kukaribia kwa uchanguzi mkuu wa urais ambao unawahusisha watu mashuhuri,rais Robert Mugabe na mpinzani wake mkuu Morgan Tvsangirai pamoja na Simba Makoni.
Kumekuwa na madai ya upande wa upinzani kuwa upande wa Mugabe unapanga kuibia,madai ambayo yamekanushwa.Yeye Mugabe amesema hatatoa madaraka kwa wapinzani akiwa baado hai.
Polisi ya Zimbabwe inamshikilia rubani mmoja wa ndege ya Helikopta baada ya kutua katika uwanja mdogo wa ndege wa Charles Prince wa mjini Harare.
Rubani huyo ambae anakaa Johannesburg Afrika Kusini,alikuwa amsafirishe kiongozi wa upinzani wa chama cha Movement for Democratic Change-MDC, Morgan Tvsangirai katika mikutano mbalimbali ya kampeini nchini humo.Ndege hiyo imekamatwa.
Mshauri mmoja wa mgombea mwingine wa urais Simba Makoni amesema kuwa nao pia walikuwa wamewasiliana na rubani huyo,ili kumpeleka katika eneo la Victoria Falls lakini waliamua kumuacha baada ya Makoni kuamua kubadili mikakati yake ya kubobea mjini Harare.
Polisi ya Zimbabwe ilikuwa itoe tarifa kuhusu kumatwa kwa rubani huyo pamoja na ndege yake.
Mchambuzi mmoja wa serikali ameliambia gazeti la Zimbabwe la Herald kuwa rubani huyo ambe ana pasi ya kusafiria ya Uingereza,ametumwa na mkoloni wa zamani wa nchi hiyo,Uingereza kumpiga jeki Tvsangirai katika kampeini zake za kuwania urais.
Chama tawala cha Zanu PF kinadai kuwa Tvsangirai ameliambia gazeti la Uingereza la The Wall Street Journal kuwa endapo atashinda uchaguzi wa jumamosi atawarejeshea wazungu mashamba yao yaliyochukuliwa na utawala wa Mugabe.Mugabe akaapa kuwa Zimbabwe haiwezi kukubali kubadilika kwa serikali ambako kunaungwa mkono na mataifa ya nje.
Tvsangirai amekanusha madai ya kuwarejeshea wazungu ardhi yao ingawa amekuwa akiukosoa mpango uliojaa vurugu wa Mugabe kuhusu mashamba ya wazungu.
Mchambuzi mmoja wa masuala ya Zimbabwe, Basildon Peta, anasema kujitokeza kwa Simba Makoni kumpa changamoto rais Mugabe ni sura mpya katika chama tawala.
Kwa mda huohuo upande wa upinzani nchini humo jumatano umerejelea hofu ya jamii ya kimataifa kuwa huenda uchaguzi ujao usiwe huru na wa haki,licha ya hakikisho la serikali kuwa utakuwa huru.
Watu wawili ambao wamejitokeza kumpinga Mugabe katika uchaguzi huo,Morgen Tvsangirai na Simba Makoni wamemlaumu Mugabe na chama chake cha ZANU PF kwa kujaribu kuibia kura kwa kutumia vyombo vya dola kuwanyanyasa wapiga kura na kuwanyima mwanya wapinzani katika vyombo vya habari. Aidha shirika la Amnesty International limetoa taarifa jumatano ambapo linasema kuwa wapinzani wananyanyaswa.