Uchaguzi mkuu wafanywa nchini Zimbabwe
29 Machi 2008Kiasi ya Wazimbabwe milioni 6 wameandikishwa kupiga kura,huku Rais Robert Mugabe akikabiliwa na kile kinachosemekana kuwa ni changamoto kali kabisa tangu kiongozi huyo kushika madaraka miaka 28 iliyopita.
Mugabe anapambana na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha MDC,Morgan Tsvangirai na vile vile waziri wake wa zamani wa fedha,Simba Makoni alieondoka chama tawala cha Mugabe ZANU-PF.Viongozi hao wa upinzani wamelalamika kuwa Mugabe ana njama ya kufanya udanganyifu wa kura.Tsvangirai amesema,chama chake kimepata ushahidi wa udanganyifu mkubwa wa kura ikiwa ni pamoja na majina ya kubuniwa katika orodha ya wapiga kura,kaskazini mwa Zimbabwe.Mugabe amepinga tuhuma hizo.
Wazimbabwe wengi wanalalamika kuhusu hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo,ambayo hapo zamani ilikuwa na uwezo wa kulisha mataifa mengine barani Afrika.Hivi sasa,Wazimbabwe wanapambana na mfumuko wa bei uliopindukia asilimia 1000 na idadi ya watu wasio na ajira ni zaidi ya asilimia 80
Vituo vya kupigia kura vinatazamiwa kufungwa saa moja usiku.Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi hayatarajiwi kabla ya Jumapili na itachukua siku kadhaa kuhesabu kura zote zilizopigwa.Zimbabwe imewapiga marufuku wasimamizi wa uchaguzi kutoka nchi za Magharibi.
Hakuna ripoti za machafuko makubwa,lakini polisi imesema, nyumba ya mgombea ubunge wa chama tawala,Judith Mkwanda imeshambuliwa kwa bomu la petroli katika mji wa kusini wa Bulawayo.