1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu nchini Tunisia Jumapili.

Mohammed AbdulRahman21 Oktoba 2004

Wakosoaji wanasema bado kuna vipingamizi vikubwa kuelekea demokrasia.

https://p.dw.com/p/CHiC
Rais Zine al-Abidine Ben Ali (Kulia)akizungumza na waziri wa nje wa Ujerumani Joscka Fischer wakati Bw. Fischer alipokua ziarani mjini Tunis Mei mwaka jana.
Rais Zine al-Abidine Ben Ali (Kulia)akizungumza na waziri wa nje wa Ujerumani Joscka Fischer wakati Bw. Fischer alipokua ziarani mjini Tunis Mei mwaka jana.Picha: AP

Tunisia itakua na uchaguzi wa bunge na Rais jumapili ijayo-uchaguzi ambao wadadisi wanasema unaonekana utakua ni pigo jengine katika juhudi za kuleta demokrasia ya kweli katika taifa hilo la Afrika kaskazini. Hoja hiyo inazungumzwa pia na chama cha upinzani cha demokrasia ya kijamii kwa ajili ya uhuru na kazi, kinachoongozwa na Mutsapha Ben Jaafar.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo wa upinzani ni kwamba bado hakuna uwazi na uhuru wa kweli wa kisiasa chini ya mfumo wa vyama vingi nchini Tunisia, na hali hiyo inazusha shaka shaka kama kweli kwa mara nyengine tena uchaguzi wa bunge na rais Jumapili utakua wa kidemokrasi.Serikali ya rais Zine al-Abidine Ben Ali inasema Tunisia iliojipatia uhuru kutoka kwa wafaransa 1956, inaelekea kwenye demokrasia kwa sababu uchaguzi wa Rais Oktoba 24 mwaka huu, unagombwa na Rais Ben Ali na wapinzani watatu kutoka vyama vya kisiasa ambavyo ni halali, na hilo pekee ni ushahidi wa kutosha.

Kwa mujibu wa maafisa wa kibalozi wa nchi za kigeni, kutopiga hatua kubwa katika suala la demokrasia kwa Tunisia, kunaziweka nchi za magharibi na hasa hasa Marekani ,katika hali ngumu kwa kuwa zinataka paweko na demokrasia yenye upeo mpana zaidi katika ulimwengu wa kiarabu, wakati huo huo ikivutia washirika katika vita dhidi ya ugaidi.

Rais Ben Ali alisimama kama mgombea pekee katika uchaguzi wa 1989 na 1994 na akakabiliana na wapinzani wawili katika uchaguzi wa kwanza kuwa wazi 1999 ambapo Ben Ali alitangazwa mshindi kwa zaidi ya 99 asili mia ya kura-tarakimu ambazo wakosoaji wanasema zilikua ni kichekesho kufuatia ahadi ya kwamba uchaguzi ungekua huru na wa haki. Katika kura ya maoni kuhusu katiba mpya 2002, Ben Ali akapata uungaji mkono mwengine wa 99 asili mia ya kura, na hivyo kupewa kibali cha kuweza kuendelea kubakia madarakani hadi 2014, iwapo ataamua kugombea tena 2009.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha demokrasia ya kijamaa kwa ajili ya uhuru na kazi Mustapha Ben Jaafar anasema, kutokana na kufanyiwa mizengwe katiba 2002 na ukosefu wa hali ya kuweza kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki pamoja na ukosefu wa uwazi wa kisiasa, hata uchaguzi wa jumapili utakua ni pigo jengine tu litakaloongezea hesabu ya matukio ya siku za nyuma.

Hata hivyo Wafuasi wa Rais Ben Ali wanasema kiongozi huyo ni maarufu kwa sababu, ameleta utulivu wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mamilioni ya watunisia katika eneo ambaloni la misukosuko na ukosefu wa haki sawa.

Lakini wakosoaji wanaishutumu serikali kwa kuhodhi vyombo vya habari kwa miaka mingi, na kuwapa wapinzani muda mchache tu wakati wa kampeni rasmi ya uchaguzi ilioanza tarehe 10 ya mwezi huu. Ben Jaafar anasema hapawezi kujengwa demokrasia ya kweli nchini Tunisia , wakati ambapo kwa muda mrefu sasa hakuna uhuru wa vyombo vya habari na wala vyombo huru vya kisheria. Katika hali hiyo anasema mwanasiasa huyo, matakwa ya raia hayawezi kupewa nafasi. Akauliza nani ameusikia upande wa upinzani ? Akiongeza kwamba chama chao hakikupata nafasi hata ya dakika moja katika televisheni na Redio, tangu pale kilipohalalishwa 2002.

Wachambuzi nao wanasema watunisia wengi wahamjui mtu mwengine anayegombea Urais, zaidi ya rais Ben Ali, ambaye wanamshutumu kwa kuunda taifa linaloendeshwa kwa ukaguzi wa vyombo vya dola vya usalama, baada ya kuchukua wadhifa huo kutoka kwa rais wa kwanza Habib Bourguiba 1987.Picha za Ben Ali zinaonekana kila mahala kwenye mji mkuu Tunis na huonekana kila siku katika kurasa za usoni za magazeti.

Wakosoaji nje ya Tunisia ikiwa ni pamoja na kituo cha kuwalinda waandishi habari chenye makao yake makuu mjini Newyork, Shirikisho la kimataifa la waandishi habari lililoko mjini Brussels na mashiriaka yanayotetea haki za binaadamu Human rights Watch na Amnesty International, yameikosoa serikali kwa kuvikandamiza vyombo vya habari na ukiukaji wa haki za binaadamu.Kadhalika magazeti na majarida ya kigeni huchunguzwa na makala zinazokosoa serikali huzuiwa na vyombo vya dola.

Kiasi ya watu maarufu na wanasiasa jumla ya 800 wengi kutoka vyama sita vya upinzani wanagombea uchaguzi wa bunge, linalothibitiwa kwa zaidi ya 80 asili mia na wanachama wa chama cha RCD cha Rais Zinne al-Abidinne Ben Ali. Ben Ali binafsi ana wapinzani watatu katika uchaguzi wa Rais.