Uchaguzi Guinea.
28 Juni 2010Katika zoezi la jana, ambapo raia wa Guinea wapatao milioni 4.2, wenye uwezo wa kupiga kura walijitokeza kumchagua mgombea mmoja kati ya 24 kwa ajili ya kiti hicho cha Urais, idadi kubwa ya watu walishiriki katika uchaguzi huo, ambao umefanyika miezi tisa tu baada ya kutokea machafuko ya umwagaji damu yaliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo chini ya utawala wa kijeshi dhidi ya wapinzani. Watu 156 waliuawa katika mkasa huo.
Watu walioshuhudia tukio hilo muhimu jana, akiwemo kiongozi wa kituo kimoja cha kupiga kura mjini Conakry, Abdoulaye Sylla, wamekiri kujitokeza watu wengi na kwamba mpaka zoezi hilo linamalizika hakukuwa na matatizo yoyote, licha ya kutokea matatizo ya hapa na pale, ukiwemo uhaba wa vifaa vya upigaji kura.
Aidha baadhi ya watu waliohojiwa wakati wa uzoezi hilo la kupiga kura walionesha nia yao ya kumchagu mtu mwenye uwezo wa kuendesha nchi bila ya upendeleo kwa kusema kuwa hawachagui rais kwa kuangalia chama chake au kabila, lakini kwa kuangalia uwezo wa mgombea na nini atakachoweza kuwaletea watu wa Guinea.
Waangalizi wa kigeni katika uchaguzi huo, wakiwemo kutoka Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Jumuia ya Uchumi ya nchi za Afrika magharibi -ECOWAS- wamesifu msimamo walioonesha wapiga kura wa Guinea kwa kujitokeza kwa wingi na kwa utulivu na amani kuamua hatima ya baadaye ya nchi yao.
Raia wengine wa nchi hiyo wapatao 120,000 walijiandikisha kupiga kura katika nchi zipatazo 17, zikiwemo Sierra Leone na Senegal.
Na matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa kuanzia Jumatano, wakati matokeo kamili yakitarajiwa katika kipindi cha siku saba.
Kati ya wagombea hao 24 waliojitokeza, mawaziri wakuu wa zamani wa nchi hiyo, Cellou Dalein Diallo, na Sidya Toure pamoja na kiongozi wa zamani wa upinzani, Alpha Conde, wanaonekana kuelekea kushinda.
Akizungumza na wafuasi wake, mgombea katika uchaguzi huo wa jana wa urais nchini Guinea, Cellou Diallo, amesema wanapaswa kuheshimu matokeo, hivyo atayakubali matokeo yoyote yatakayotolewa.
Na kiongozi wa serikali ya mpito ya Guinea, Sekouba Konate, akipiga kura yake hapo jana, alikumbushia ahadi yake aliyoiweka hapo kabla ya kuifikisha nchi hiyo katika uchaguzi wa kidemokrasia na ulio wazi, na kutoa wito wa kuwapo na umoja na mshikamano.
Tangu koloni hilo la zamani la Ufaransa lilipojipatia uhuru mnamo mwaka 1958, Guinea, nchi ya kwanza kati ya nchi zinazosafirisha kwa wingi zaidi maadini ya Beauxite ulimwenguni, imekua ikishuhudia tawala za chama kimoja au tawala za kijeshi.
Mara tu baada ya Guinea kupata uhuru, nchi hiyo iliongozwa na Ahmed Sekou Toure, aliyetawala kwa miaka 26 mpaka alipofariki mwaka 1984, ambapo palitokea mapinduzi yaliyouweka madarakani utawala wa kijeshi chini ya uongozi wa Lansana Conte, aliyetawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 24 mpaka alipofariki dunia mwaka 2008 na haraka kufanyika tena mapinduzi.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp)
Mhariri: Miraji Othman