Uchaguzi Ethiopia
24 Mei 2010Matangazo
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini
Ethiopia wa Medrek, Merara Gudina,
ameyaelezea matukio kadhaa yanayohusishwa
na udanganyifu wakati wa zoezi hilo la upigaji
kura katika mji wa kusini wa Oromiya ambao ndio
ngome kuu za upinzani pamoja na mji wa Ambo.
Amesema haukuonesha kama ni uchaguzi, hata
kwa viwango vya Afrika na kwamba hakuna sheria
yoyote inayowalazimisha wao kukubali matokeo
yoyote na kuongeza kwamba anazotaarifa kuwa
visanduku vya kupigia kura viliongezwa.
Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2005 rekodi
iliyowekwa na vyama vya upinzani ilionekana
kuwa nzuri zaidi, hali ambayo ilipelekea kutokea
ghasia zilizosababisha vifo vya watu 200, huku
serikali ikichukua hatua kali zilizosababisha
viongozi muhimu wa upinzani kutupwa gerezani,
kukimbilia uhamishoni na wengine kumalizwa
nguvu zao kisiasa.
Naye Mwenyekiti wa sasa wa muungano huo wa
upinzani, Beyene Petros, amesema ushindi
unaweza kutangazwa tu, kupitia wizi wa kura na
si vinginevyo.
Kwa upande wake, kiongozi wa waangalizi wa
uchaguzi huo kutoka Umoja wa Ulaya,Thijs
Bergman, ameupongeza uchaguzi huo kwa kuwa
na amani na utulivu, huku tume ya taifa ya
uchaguzi nchini humo ikisema kuwa hakuna
ushahidi wowote wa udanyanyifu uliofanywa licha
ya viongozi wa upinzani katika majimbo kadhaa
kulalamikia kufanyiwa mizengwe.
Hata hivyo, mkuu huyo wa waangalizi wa
uchaguzi wa Umoja wa Ulaya amesema
wamesikia kilio hicho cha upinzani na kwamba
wanafanyia uchunguzi madai hayo.
Umoja wa Ulaya umetuma waangalizi wake
wapatao 160 katika uchaguzi huo wakati Umoja
wa Afrika wakipeleka waangalizi 60, ambapo
wapiga kura wapatao milioni 32 jana walichagua
wabunge 547 na madiwani.
Matokeo ya majimbo yatatangazwa kesho huku
matokeo rasmi ya mwisho yakisubiriwa
kutangazwa katika mwezi mmoja ujao.
Katika nchi hiyo ambayo viongozi wengi
mashuhuri wa upinzani wako gerezani na
mashirika ya haki za binadamu yakikosoa
kutokana na kunywea uhuru wa kisiasa wakati wa
kampeni, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles
Zenawi, amepuuza malalamiko hayo yaliyotolewa
na upinzani na kusema kuwa anategemea kupata
ushindi ili kuendelea kuuimarisha uchumi wa wa
nchi hiyo.
Mwandishi Halima Nyanza(afp)
Mhariri: Miraji Othman
Matangazo