1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Australia

Ramadhan Ali23 Novemba 2007

Hatima ya waziri mkuu Howard yaamuliwa leo iwapo asalie madarakani au la.

https://p.dw.com/p/CSRJ

Wananchi wa Australia, wanapiga kura hii leo (jumamosi) kuamua hatima ya utawala wa miaka 11 ya waziri mkuu John Howard. Howard, amesema yutayari kuridhia matokeo yoyote ya uchaguzi wa leo . Uchunguzi wa maoni, unampa ushindi wazi kiongozi wa upinzani wa chama cha Labour, Kevin Ruud.Uchaguzi huu ulitanguliwa na kuuwawa jana kwa askari mwengine wa Australia nchini Afghanistan,mojawapo ya mada za kampeni kali iliotangulia uchaguzi wa leo.

Katika kilio chake cha mwisho kuwanasihi wapiga kura kumrejesha madarakani,waziri mkuu John Howard wa chama cha Conservative alionya jana kuwa Australia itabadilika mno ikiwa utawala wake wa miaka 11 utakoma.

Kiongozi wa upinzani wa chama cha Labour,Kevin Ruud, amekuwa akiongoza usoni kabisa katika kura ya maoni.Biramu lake la uchaguzi lilikuwa ni kukaribisha kizazi kipya cha uongozi na kuahidi pia kutia saini mkataba wa Kyoto wa kuzuwia kuchafuka kwa hali ya hewa na kuyondoa majeshi ya Australia nchini Iraq.

Baadhi ya magazeti maarufu ya Australia,yamewataka wapigakura kuwampiga kumbo waziri mkuu Howard na uchuzi wa aina 2 umebainisha ushidi kwa chama cha Labour.

Bw.Howard na Ruud walipojitosa katika hatua ya mwisho ya kampeni katika mijadala ya TV na radio, uchunguzi wa kituo cha AC Nielsen, umekipa chama cha Labour uongozi wa 14% ya kura –matoeko ambayo yatakitimua madarakani chama cha Conservative cha waziri mkuu Howard.

Uchunguzi wa kituo kingine cha maoni-Galaxy umesema chama cha Labour chaongoza kwa 4% tu matokeo ambayo yatakikaribisha chama-tawala cha conservative karibu na Labour kwa mara ya kwanza.

Chama cha Labour, kinahitaji kunyakua viti 16 zaidi ili kuparamia madarakani.Chochote kitakachotokea,huu utakuwa uchaguzi wa mwisho kwa waziri mkuu Howard ,mshirika wa chanda na pete wa rais George Bush na aliekua waziri-mkuu wa Uingereza Tony Blair katika vita vya Iraq.

Howard akiwa na umri wa miaka 68 ameahidi kustaafu na kumkabidhi hatamu za uongozi makamo wake Peter Castello baada ya kupita kipindi cha miaka 2.

Waziri mkuu Howard alitumia siku ya mwisho ya kampeni,akijitenga na vipeperushi-bandia vilivyoenezwa dhidi ya waislamu.Vipeperushi hivyo vimeenezwa na wafuasi wa chama chake katika jimbo muhimu sana la uchaguzi mjini Sydney.

Inahofiwa vinaweza vikamharibia Howard nafasi zake za ushindi.

Kiongozi wa Upinzani Kevin Ruud,mwenye umri wa miaka 50, mjumbe wa zamani wa kibalozi, ameahidi mapinduzi katika sekta ya elimu na kubadili sheria za kazi zilizoleta mabishano.

Howard amefanya kampeni akiegemea zaidi jukwaa la uchumi bora unaozidi kukua n a ukosefu mdogo kabisa wa kazi nchini.Ikiwa pigo kwake, magazeti makubwa na maarufu ya Australia jana yaliwataka wapiga kura milioni 13.6 kumbwaga chini waziri mkuu Howard na kumchagua kiongozi wa Labour Kevin Ruud.

Akianguka Howard,mshirika mwengine wa George Bush katika vita vya Irak,baada ya waziri-mkuu Aznah wa Spain;Balusconi wa Itali,Tony Blair wa Uingereza,ataliacha jahazi la Bush linalokwenda mrama.