1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubalozi mdogo wa Ujerumani, washambuliwa Afghanistan

11 Novemba 2016

Kiasi ya watu sita wameuwawa na wengine 100 kujeruhiwa kufuatia shambulizi la mabomu ya kutegwa ndani ya Lori lililofanywa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga mbele ya ubalozi mdogo wa Ujerumani, mjini Mazar-i-Shariff.

https://p.dw.com/p/2SXWq
Afghanistan deutsches Generalkonsulat in Masar-i-Scharif
Picha: picture-alliance/dpa/N. Armer

Kikundi cha wapiganaji wa Taliban kimedai kuhusika na shambulizi hilo kwenye ubalozi huo mdogo ulioko mji wa Mazar-i-Shariff, Kaskazini mwa Afghanistan. 

Wapiganaji wa Taliban waliegesha lori lililokuwa na mabomu kwenye ukuta unaozunguka ubalozi huo mdogo wa Ujerumani katika mji wa Mazar-i-Sharif, jana usiku na kusababisha mauaji ya kiasi ya watu sita na wengine wakajeruhiwa , maafisa wa Taliban wamesema.

Kufuatia shambulizi hilo, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Stainmeier ameitisha kikao na kikosi cha kukabiliana na majanga kilichopo ndani ya wizara hiyo ili kwa pamoja kujadili hali ilivyo.

Msemaji wa Gavana wa jimbo la  Balkh, ambako kunapatikana ubalozi huo aliyejulikana kwa jina moja, Munir amesema raia mmoja wa eneo linapopatikana ubalozi aliripoti kusikia mripuko mkubwa uliofuatiwa na milio ya risasi. Mripuko huo ndio uliosababisha kutawanyika kwa vigae  vya majengo yaliyoharibiwa  yaliyokuwa jirani na ubalozi na kuwajeruhi wengi.    

Ofisi ya mambo ya nje ya Ujerumani imeripoti shambulizi hilo kufanywa ndani na nje ya ubalozi huo mdogo wa Ujerumani na kuongeza kuwa vikosi kutoka Afghanistan na kikosi cha  NATO walikuwepo kwenye tukio hilo. Vikosi hivyo baadae viliripoti kumalizika kwa shambulizi hilo.

Afghanistan Explosion in der Nähe des deutschen Konsulatsbüros in Mazar-i-Sharif
Askari waliowasili kwenye eneo la ubalozi lililoshambuliwa wakiendelea kufanya uchunguzi.Picha: Reuters/A. Usyan

Maafisa wa Afghanistan na madaktari wamesema zaidi ya watu 100 walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo. Mshambuliaji mmoja aliuwawa kwenye shambulizi. Msemaji wa ofisi ya masuala ya nje ya Ujerumani amesema watumishi wote wa ubalozi huo walikuwa salama na hawakudhurika na shambulizi hilo, ingawa jengo la ubalozi liliharibiwa vibaya.

Mkuu wa jeshi la polisi kwenye jimbo la Balkh ambako tukio hilo limetokea, Saied Kamal amesema kulionekana mshambuliaji mmoja tu aliyehusika. Hata hivyo baadae mamlaka zilieleza kumbaini mshambuliaji mwingine aliyefunikwa na kifusi cha matofali. Ofisi ya masuala ya nje ya Ujerumani, iliripoti kuzuiwa kwa washambuliaji hao na vikosi vya usalama, ingawa haikutaja idadi yao halisi. Kiasi ya wanajeshi 900 wa Ujerumani walipelekwa eneo hilo kuhakikisha usalama.

Kikundi cha wapiganaji wa Taliban kimeeleza kuhusika na shambulizi hilo, kwa madai ya kulipiza kisasi kufuatia shambulizi la anga lililofanywa Novemba 3 na majeshi ya NATO karibu na Kaskazini mwa mji wa Kunduz na kusababisha mauaji ya raia. Mapema mwezi huu, Jeshi la Marekani lilieleza kuanzishwa kwa uchunguzi wa shambulizi hilo la anga ambalo lilisababisha vifo na majeruhi kwa raia.

Maafisa wa Taliban walisema, raia 33, ambao ni pamoja na watoto 17 walikufa kufuatia shambulizi hilo la anga, na wengine 26 kujeruhiwa. jamaa ya wahanga hao waliandamana hadi nje ya jengo la gavana wakilaani shambulizi hilo. 

Mwandishi: Lilian Mtono/  http://www.dw.com/en/german-consulate-in-afghanistan-attacked-with-taliban-car-bomb/a-36351272/ AFP 
Mhariri: Saumu Yusuf