1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubakaji ni kosa la kivita

Nijimbere, Gregoire20 Juni 2008

Umoja wa mataifa umesema vitendo vya kuwanyanyasa wanawake kwa ngono katika maeneo ya vita ni kosa la kivita na sehemu ya mauaji ya kuangamiza jamii. Azimio limepitishwa kukomesha ukatili huo dhidi ya wanawake

https://p.dw.com/p/ENgG
Mhanga wa ubakaji Mukhtar Mai kutoka Pakistan akielekea MarekaniPicha: AP

Wajumbe kwenye kikao hicho cha Baraza la usalama la Umoja wa mataifa kilichokuwa kikiongozwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleeza Rice, wamesema ubakaji na ukatili mwingine wa ngono vinavyotendewa wanawake ni kosa la kivita, kosa dhidi ya binaadamu au mmoja ya vitendo vya kuangamiza jamii. Azimio hilo numbari 1820 linatishia vile vile kuwapeleka mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na ubakaji.

Mwenyekiti wa kikao hicho cha Baraza la usalama la Umoja wa mataifa, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleeza Rice alisema kuwa ubakaji ni kosa ambalo haliwezi kufumbiwa macho.

Na baada ya wajumbe wote 15 kupitisha azimio, Rice alielezea furaha yake kwa kusema:

"Ninasikia fahari leo kwa kuwa tumelijibu vizuri swala lile linalokera kwa kusema ndio"


Kwani maelezo mengi yalikuwa yametolewa kwenye mkutano huo wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu madhara ya vitendo hivyo vya kuwanyanyasa wanawake kwa vitendo vya ngono.

Muakilishi wa Uingereza kwenye kikao hicho Patricia Scotland amesema vitendo kama hivyo vya ukatili wa ngono dhidi ya wanawake ni kikwazo kwa juhudi za amani kwa jumla.

"Kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa ngono dhidi ya wanawake ni hatari na ni kitisho kikubwa kwa amani na usalama"


Azimio hilo linalokomesha vitendo vya kuwanyanyasa wanawake kwa ngono, limekaribishwa na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, limetoa taarifa ambamo limesema azimio hilo la Baraza la usalama la Umoja wa mataifa ni hatua kubwa na la kihistoria katika taasisi ambayo mara nyingi imeonekana kutofahamu usumbufu unaowakabili akinamama na wasichana katika sehemu za mapigano.

Kwa sasa ni budi patengenezwe njia ya kukusanya ripoti zote juu ya vitendo hivyo viovu vinavyotendewa wanawake, limezidi kusema Human Rights Watch.Nchi za Myanmar, Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na Sudan zilitolewa kuwa mfano mbaya wa sehemu za dunia ambako vitendo vya ukatili wa ngono dhidi ya wanawake vimekithiri.