UAMUZI WA KUIPA VIFARU VYA 'FUCHS' IRAQ NA MVUTANO NDANI YA CHAMA CHA CDU NDIO MADA KUU :
29 Septemba 2004Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani, umetuwama hasa juu ya uamuzi wa serikali ya Ujerumani kuipa Iraq magari ya uchukuzi ya vifaru chapa ‘FUCHS’ ,mipango ya mageuzi ya chama kikuu cha upinzani CDU kuhusiana na kinga ya mtu kufukuzwa kazini na marekebisho ya kiuchumi katika Kampuni la maduka la KARSTADT-QUELLE.
Kuhusu tangazo la serikali ya ujerumani kuipelekea Iraq magari ya aina ya vifaru ya usafiri chapa FUCHS,linauliza gazeti la DIE WELT:
"je, serikali ya muungano wa vyama vya kijamaa –SPD na walinzi wa mazingira-KIJANI inapoteza sasa sifa yake ya kutouza silaha katika maeneo ya migogoro ? Mpango wa kuipa Iraq vifaru hivyo 20 katika hali ya vita kunaweza kutoa sura hiyo....kwani magari hayo ya vifaru hayatatumika kuisafirisha timu ya mpira ya Iraq huko baghdad bali yatatumika kusafirishia wanajeshi waliojizatiti kisilaha kupita njia walimojizatiti wafyatuaji risasi na waliotega mabomu. Magari ya chapa Fuchs ni wazi kabisa ni zana za vita na hivyo serikali ya Ujerumani inakuwa sasa kigeugeu-inazungumza hivi inafanya vyxengine.Kwani ni magari haya haya ambayo,haitaki kuipa Israel kwavile ingeyatumia huko dhidi ya wapalestina,lakini Irak haidhuru kitu’-lamaliza gazeti-DIE ZEIT.
Tukigeukia siasa za ndani ya Ujerumani,nia ya chama kikuu cha Upinzani CDU endapo kikija madarakani kitaregeza sheria ya kuwalinda wafanyikazi kutimuliwa makazini ovyoovyo, ili kuweza kukuza uchumi na nafasi za ajira, gazeti la TAGES ZEITUNG kutoka Munich laandika:
"mwenyekiti wa chama cha CDU bibi Angela Merkel bila ya shaka ana matatizo.Ili kuwavunja nguvu mahasimu wake kwamba hajitengi mno kabisa kutoka sera za Kanzela Schröder,Bibi Merkel sasa mefunga kibwebwe kugeuza mno mkondo wa sera zake kwa kadiri ambayo anavuka mpaka.Kufanya kazi bila kikomo,kutokua na sauti ya kuamua pamoja makazini na hata haki ya kufanyakazi sio siku nzima anapanga kuifuta.Kinachoidhi mno katika sera zake hizo za kuwafurahisha waajiri ni kwamba hakutasaidia kutoa nafasi mpya za kazi bali kutamfufulia matataizo mapya." Hilo lilikua Tageszeitung kutoka Munich.
Gazeti jengine la TAZ linalochapishwa Berlin, linayaona mashauri ya chama cha CDU hayapendezi kabisa.Laandika:
"Ni uzuri kuona jinsi gani wanachama wa CDU wanavyobishana tena hadharani kuhusu maswali tangu ya viongozi hata mkakati. lakini wananchi ambao hawapendezwi na serikali,wanasubiri kitambo sasa bila ya jibu kusikia mashauri bora kutoka Upinzani.Badala yake wanapewa mseto kati ya kuwapunguzia haki zao wafanyikazi na ruzuku zinazolipwa wanyonge kwa matumizi ya mbinu zile zile za zamani zilizopitwa na wakati.
Nini jibu lao wananchi ,wameliona kutoka chaguzi za wiki chache zilizopita,kwani wengi wao waliamua kujikalia majumbani mwao bukheri-mustarehe na kutokwenda kutia kura."Hilo lilikua TAZ kutoka Berlin.
Hata gazeti la biashara-HANDELSBLATT kutoka Düsseldorf,halioni mbinu ya kijamii,kisiasa na kiuchumi kutoka vyama vya muungano wa CDU na CSU.
Gazeti laandika:
"Wiki hizi zijazo itaamuliwa iwapo CDU itamudu kutupa turufu nzito mezani.Chama hiki kinakabiliana na changamoto kali chamani katika historia ya chama.Umuhimu wa changamoto hiyo ni vigumu sana kuitoa maanani hata ikiwa juu kwa juu yaonekana maswali yanayobishaniwa ni ya mageuzi.Kwani hivi sasa uamuzi wa mwanzo utakatwa iwapo chama hiki cha CDU kitaingia katika uchaguzi mkuu ujao kama serikali barabara na bora kuliko hii ya sasa ya chama cha SPD na KIJANI au la."
Mwishoe, gazeti la FINANCIAL TIMES la Ujerumani latubadilisha mada likigeukia mkondo uliochukuliwa na kampuni kubwa la maduka la Ujerumani-KARSTADT-QUELLE kusafisha hazina yake:
Gazeti laandika kwamba, ni hatua ya kujikomboa aliopiga bosi wa kampuni hilo Bw.Christoph Achenbach.swali lakini ni je, atamudu kulizuwia jahazi lake hili kweli lisiende mrama na mwishoe kuzama ?Bw.Achenbach na zaidi mkuu wa bodi ya kampuni hili Thomas Middelhoff wameamua kupitisha ufagio barabara .Wamepanga maduka yote madogo-madogo ya Karstadt yenye neo la chini ya mita 8000 za mraba,yatokomee.Hata pia maduka yake ya nguo ya Sinn-Leffers,runners Point pamoja na hisa zake katika kampuni la Starbuck, kuaachana nayo.Yabainika kwamba, maalfu ya nafasi za kazi yatapotea.Kwa jicho la hali ya msukosuko inayojikuta Karstadt-Quelle hatua hizo zote haziepukiki laandika gazeti.