Uamuzi wa Bahari ya Kusini mwa China waipa nguvu Ufilipino
13 Julai 2016Mahakama ya Kimataifa ilitoa uamuzi mkali dhidi ya China hivi karibuni kuhusiana na eneo linalozozaniwa la bahari ya kusini mwa China, baada ya Ufilipino kuwasilisha kesi yake katika mahakama hiyo. Eneo ambalo kwa hakika, China inalizozania dhidi ya mataifa kadhaa mengine ya barani Asia ikiwa ni pamoja na Vietnam, Taiwan, Malaysia na Brunei.
Lakini wachambuzi wanasema, uamuzi huo hautarajiwi kuleta mabadiliko makubwa katika sera ya China ya kujitanua katika mpaka wa bahari. Suala linaloibuka sasa, ni je China kweli itafuata maelekezo ya uamuzi huo?
Ingawa China inasisitiza kuwa haiutambui uamuzi wa Mahakama ya kudumu ya sheria inayoshughulikia migogoro yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi, wachambuzi wanasema Ufilipino imejipatia nguvu sasa ya kuweza kujadiliana na China juu ya ene hilo. Pia wachambuzi hao wanaonya hii ni hatua ya kwanza tu, kuelekea kazi kubwa inayohitajika kufanywa ili kuusuluhisha mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa.
"Changamoto iliyopo sasa, ni jinsi ya kuugeuza ushindi mdogo uliopatikana kuwa sera iliyo imara itakayoweza kusuluhisha mgogoro huu unaoendelea barani Asia," amesema Lauro Baja, balozi wa zamani wa Ufilipino kwa Umoja wa Mafaifa.
"Ni hatua iliyozipa pande zote mbili nafasi ya angalau kupunguza makali ya mvutano uliopo baina yao, na kuweza kuanza mazungumzo," ameongeza Baja.
China yadai kuwa na haki ya kihistoria
China imejenga miradi ya ardhi ikiwamo visiwa bandia katika Bahari ya Kusini mwa China, ujenzi unaoweza kugeuka kuwa vituo vya kijeshi katika eneo kuu linalotumika kwa ushafirishaji wa bidhaa.
Halikadhalika imefunga njia za kuelekea eneo maalumu la jadi linalotumiwa kwa uvuvi na Wafilipino, licha ya kwamba Ufilipino ndiyo iliyo na haki zaidi kutokana na kwamba eneo hilo liko ndani mpaka wa maili 200 wa eneo lake la kiuchumi.
China inadai kwa mujibu wa historia ina haki zaidi katika Bahari ya Kusini mwa China kwa asilimia 90, ndani ya eneo lilo na utajiri wa madini na rasilimali za baharini.
Lakini mahakama imesema kwa misingi ya kisheria, China haiwezi kudai umiliki kupitia haki za kihistoria. Mahakama pia imethibitisha Ufilipino ina haki kamili katika eneo lake ilotengewa la Bahari ya Kusini mwa China, na kwamba aneo hilo haliingiliani na eneo la China.
Ujenzi wa China waharibu mazingira
Mchambuzi wa kisiasa na ulinzi Clarita Carlos, amesema China inalazimika kuchukua hatua za kuupunguza mvutano uliopo katika Bahari ya Kusini mwa China.
"Kupoteza heshima kwa China ni jambo la aibu sana, na haitaki kuaibika mbele ya jumuiya ya kimataifa," Carlos ameliambia shirika la habari la dpa. "Lakini kwa vyovyote vile, lazima ichukuwe hatua, lazima isitishe ujenzi wake wa visiwa bandia pamoja na uharibifu wa miamba ya matumbawe, ambao kwa hakika unaathiri kila mtu."
China kwa upande wake imegoma kuutambua uamuzi wa mahakama ya kimataifa, hata hivyo imesema iko tayari kufanya kazi na nchi nyengine za pwani pamoja na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha usalama pamoja na uhuru wa meli ya kusafirisha bidhaa katika Bahari ya Kusini mwa China.
"China inaheshimu uhuru wa mataifa yote katika Bahari ya Kusini mwa China chini ya sheria ya kimataifa," Wizari wa Mambo ya Nje imeandika katika taarifa yake.
"Wavuvi wa Ufilipino wanaweza kubahatisha kuingia katika maeneo ambayo yamewekewa vizuizi na China, ili waone kama kuna lolote lilobadilika tokea kutolewa uamuzi wa mahakama," amesema Baja.
Baja ameshauri si vibaya wakijaribu, ili waone walinzi wa majini wa China wataikubali vipi hatua hiyo.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae
Mhariri: Mohammed Khelef