Majaji wa ICC, leo watatoa hukumu kusu Rais Bashir
6 Julai 2017Hukumu ya leo itafuatiliwa kwa karibu kutokana na madhara inayoweza kuwa nayo kwa Bashir na viongozi wengine walioko madarakani na vilevile kwa korti hiyo yenyewe. Ikiwa ICC itaamuwa kuwa uamuzi wa Afrika Kusini kumuachia Bashir kuondoka kilikuwe kitendo cha ukiukaji, korti hiyo inaweza kuishitaki serikali ya Pretoria mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa au kwa wanachama wa ICC. Katika matukio yote, Afrika Kusini inaweza kupata pigo la kidiplomasia kwa kukaripiwa na Korti hiyo, na siyo kutozwa faini yoyote au kuwekewa vikwazo. Kuna uwezekano pia kwa mahakama hiyo kukubaliana na hoja ya Afrika Kusini kwamba haikuwa na wajibu wa kutekeleza waranti wa kukamatwa kwa Bashir. Afrika Kusini inahoji kwamba waranti wa ICC wa kukamatwa Bashir ulikuwa batili mbele ya sheria zake zinazotoa kinga kwa marais walioko madarakani dhidi ya kushitakiwa, kufuatana na sheria ya kimataifa. Hata hivyo sheria za ICC zinabainisha wazi kwamba marais walioko madarakani hawana kinga katika kesi za uhalifu wa kivita.