1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UAE yazindua kinu cha kwanza cha nyuklia eneo la Ghuba

1 Agosti 2020

Muungano wa Falme za Kiarabu, UAE, umezindua kinu chake cha nyuklia ambacho ni cha kwanza katika kanda ya mataifa ya kiarabu ambayo kwa sehemu kubwa inaandamwa na mizozo.

https://p.dw.com/p/3gGTN
VAE Das Akw Barakah in den Vereinigten Arabischen Emiraten
Kinu cha nyuklia cha Barakah Picha: AFP/Barakah Nuclear Power Plant

Kinu hicho kilichopewa jina la ´Barakah´ kimegharimu dola bilioni 22.4 na kimejengwa mashariki ya pwani ya mji wa Abu Dhabi na kampuni ya Kikorea.

Kitakuwa na mitambo minne ya kufua nishati ya nyuklia na kimeundwa kama mbadala wa uzalishaji nishati ya taifa hilo la Ghuba ambalo lina hifadhi ya kutosha ya mafuta lakini linawekeza katika nishati jadidifu.

Pindi kitakapokuwa kikifanya kazi kwa ukamilifu kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 5,600 za umeme, kiwango ambacho ni karibu asilimia 25 ya mahitaji ya umeme ya nchi hiyo.

Mapema hivi leo, moja ya mtambo wa kinu hicho uliwashwa na unatarajiwa kuanza kutoa nishati baadae mwaka huu.

"Kuanza kazi kikamilifu kwa kinu cha Barakah katika siku chache zijazo kutachangia juhudi za maendeleo endelevu ya Muungano wa Falme za Kiarabu" amesema Hamad Alkaabi, mwakilishi wa nchi hiyo kwenye shirika la nguvu za atomiki duniani IAEA.

Kinu cha kwanza eneo la Ghuba 

VAE Erste AKW in Barakah an das Stromnetz angeschlossen
Sehemu ya walihudhuria ufunguzi wa kinu cha Barakah Picha: picture-alliance/YONHAPNEWS AGENCY

Kinu cha Barakah ni cha kwanza kwenye kanda ya Ghuba. Taifa jirani la Saudi Arabia limetangaza mipango ya kujenga mitambo 16 ya nyuklia lakini bado hawajafanikiwa.     

Muungano wa Falme za Kiarabu taifa la nne kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta duniani, umejengwa kwa utajiri wa mapato ya mafuta na una hifadhi kubwa pia ya gesi asili.

Hata hivyo nchi hiyo inatumia mabilioni ya dola kutengeza vyanzo vipya vya nishati inayotunza mazingira ili vizalisha nusu ya mahitaji yake ya nishati ifikapo mwaka 2050.

Kinu cha nyuklia na ushawishi wa UAE

Iran Atomkraftwerk in Bushehr
Picha: picture-alliance/dpa/A. Taherkenareh

Maafisa wa nchi hiyo wanatumai kuwa pamoja na kinu hicho cha nyuklia kuzalisha nishati ya bei nafuu, pia kitaipa hadhi UAE kama taifa lenye nguvu katika eneo la ghuba na kutanua ushawishi wake kutoka Yemen, pembe ya Afrika na hata nchini Libya.

"Hii ni sehemu ya mpango wa UAE kubadili uchumi wake wa nishati, kupunguza utegemezi kwenye petroli na kujionesha káma kiongozi wa kanda hii katika sekta ya sayansi na teknolojia" amesema mchambuzi mmoja wa siasa za eneo ghuba alipozungumza na shirika la habari la AFP.

UAE imerejea mara kadhaa kuwa malengo yake ya kutumia nyuklia ni ya amani na imepuuza wasiwasi wowote kuhusu suala la usalama.

Taifa hilo limesema halitorutubisha madini ya urani au kuendeleza teknolojia ya kuunda silaha za nyuklia.