UAE kujenga bomba la mafuta kati ya Ethiopia na Eritrea
10 Agosti 2018Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE unatarajia kujenga bomba la mafuta litakalounganisha jiji la bandari la Eritrea, Assab na mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Kulingana na shirika la utangazaji lenye mahusiano na serikali nchini Ethiopia la Fana, taarifa hizo zilifichuliwa wakati wa mkutano mjini Addis Ababa kati ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na waziri anayeshughulikia mahusiano ya kimataifa wa UAE, Reem Al Hashimy.
Hata hivyo hakukutolewa taarifa zaidi, lakini Fitsum Arega, mkuu wa utumishi wa waziri mkuu Abiy ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba majadiliano na waziri Hashimy yaliangazia zaidi kwenye uwekezaji katika sekta ambazo ni pamoja na viwanda, kilimo na majengo ya kibiashara, bomba la mafuta na maeneo ya mapumziko ya kitalii.
Tangazo hili ni kiashiria cha karibuni zaidi cha Umoja wa Falme za Kiarabu kuimarisha kujihusisha kwake kwenye pembe ya Afrika.