Twitter yairejesha akaunti ya Trump
20 Novemba 2022Mtandao wa kijamii wa Twitter umeirejesha akaunti ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump. Hayo yameelezwa usiku wa kuamkia leo na mmiliki mpya wa Twitter, Elon Musk.
Akaunti ya Trump iliyokuwa imefungwa kwa muda wa miezi 22, ilionekana tena kwenye mtandao huo jana Jumamosi.
Musk aliendesha kura ya maoni, ambapo watumiaji milioni 15 wa Twitter walipiga kura, huku asilimia 51.8 wakipiga kura ya ndiyo.
Akaunti ya Trump ilisimamishwa mwezi Januari, 2021, siku mbili baada ya wafuasi wake kuyavamia majengo ya bunge la Marekani na kusababisha kikao cha bunge la pamoja kusitishwa pamoja na vifo vya watu watano.
Wafuasi hao walikuwa na nia ya kuzuia kupitishwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2020 yaliyompa ushindi Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden. Hivi majuzi, Trump alitangaza nia yake ya kugombea tena urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.
Mapema leo, Trump amesema hana haja ya kurejea kwenye Twitter na badala yake atasalia katika mtandao wake wa kijamii aliyouanzisha wa "Truth".