Twitter yahakiki ujumbe wa Trump kwa mara ya kwanza
16 Julai 2020Twitter ilichukua hatua hiyo ambayo haraka ilichochea mvutano kati yake na Trump, baada ya rais huyo wa Marekani kuandika Tweet mbili akidai kwamba mtindo wa kupiga kura kwa njia ya posta huwa una udanganyifu mwingi.
Ilichofanya Twitter, ni kuweka kiungo kingine chini ya ujumbe wa Trump kinachosema "Pata taarifa za ukweli juu ya kura ya njia ya posta,” na baadae kiungo hicho kinampeleka mtumiaji kwenye makala ya habari inayompa taarifa za ukweli kuhusu suala hilo, na orodha ya maelezo yanayopinga madai ya Trump.
Muda mfupi baada ya Twitter kuchukua hatua hiyo, Trump aliishutumu kwa kile alichokiita ‘kuingilia kati' uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba pamoja na uhuru wa kujieleza.
Trump aliandika hapo hapo katika ukurasa wake wa Twitter, kwamba mtandao huo wa kijamii unazuia uhuru wa kujieleza, na yeye kama rais hatoliruhusu hilo kufanyika. Haijulikani ni kwa namna gani Twitter itashughulikia ujumbe wa siku za mbele wa Trump ambao utakuwa unachochea kueneza taarifa za uwongo.
Je, Twitter itaendelea kukosoa jumbe za Trump?
Msemaji wa mtandao wa Twitter, Nick Pacilio, hakutoa tamko lolote kuhusu kama shirika hilo litaendelea kuhakiki ukweli wa ujumbe anaouandika Trump katika ukurasa wake wa Twitter. Mtandao huo wa kijamii wa Twitter, umekuwa ukikosolewa vikali kwa kumpa rais huyo wa Marekani uwanja wa kusambaza taarifa zisizo na ukweli.
Trump mwenye wafuasi wapatao milioni 80 katika ukurasa wake wa Twitter, anasema anautumia mtandao huo wa kijamii kupinga kile anachodai kuwa ni taarifa za upendeleo zinazotolewa na vyombo vya habari.
Trump amekuwa akidai kwamba mtindo wa kupiga kura kwa njia ya posta, una viwango vya juu vya udanganyifu, katika wakati ambapo majimbo mengi yanazingatia kuitumia njia hiyo ili kulinda afya ya raia dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19, wakati taifa hilo likiwa linaelekea katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba.
Wataalamu wa uchaguzi hata hivyo wanasema, hakuna ushahidi wa kutosha unaoashiria ongezeko la udanganyifu katika njia hiyo ya kupiga kura kupitia posta.
Mnamo mwezi Juni mwaka jana, Twitter ilisema itawajuulisha watumiaji wake juu ya ujumbe wowote utakaokiuka sera zake kama vile taarifa zinazochochea tabia ya dhuluma na usalama wa umma.