1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TWAWEZA: Wananchi wana wasiwasi na kupanda gharama za maisha

25 Agosti 2022

Utafiti mpya wa 'Sauti za Wananchi' nchini Tanzania unaoangazia gharama za maisha na tozo umebaini kuwa wananchi wengi wana wasiwasi na kupanda kwa gharama za maisha, ajira, fursa za kipato na uhaba wa chakula.

https://p.dw.com/p/4G0yK
Tansania | Aidan Eyakuze
Picha: DW/S. Khamis

Utafiti huo uliozinduliwa Alhamisi jijini Dar es Salaam na Taasisi ya Twaweza, umeonesha kuwa, mambo matatu makubwa yanayowaumiza wananchi ni kupanda kwa gharama za maisha, ukosefu wa ajira na kipato na uhaba wa chakula. Katika utafiti huo, asilimia 56 ya watu waliohojiwa, walilalamikia kupanda kwa gharama za maisha na asilimia 50 walilalamika kukosa ajira na fursa za kipato na asilimia 27 walilalamika njaa na uhaba wa chakula.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema matokeo yaliyomshangaza katika utafiti huo ni wasiwasi wa chakula kwa watu wa vijijini. Utafiti wa Twaweza, ulifanyika katika mikoa ya Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, katika maeneo ya mijini na vijijini na kuwahoji wananchi kuhusu nini mahitaji yao kwa serikali za mitaa na wananchi hao walilalamikia huduma za afya, upatikanaji wa maji safi, huduma duni za usafiri na ubora wa elimu.

Wananchi wanataka nini kwa Rais Samia

Kadhalika wananchi walihojiwa, wanataka nini kwa Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi walimtaka rais ashughulikie kupanda kwa gharama za maisha, huduma za afya na huduma za usafiri. Utafiti huo pia uliangazia gharama za tozo za simu na kupokea maoni ya wananchi kuhusu kupanda na kupunguza kwa tozo hizo.

Mshiriki katika matokeo ya utafiti huo, Edward Simbeye kutoka Chama cha NCCR Mageuzi amesema wananchi hawana budi kupewa elimu zaidi kuhusu tozo na hili lilirudishwa nyuma wakati serikali ilipozuia uhamasishaji na uchechemuzi kwa vyama vya siasa. 

Baadhi ya wachangiaji hao walisema wanasiasa Tanzania hawana budi kujifunza kuwa katiba si kipaumbele kwa wananchi na kuwa Watanzania wanahitaji chakula, wanahitaji ajira na vyanzo vya mapato. Utafiti huo uliwahoji watanzania katika kaya 3,000 na wahojiwa 3,000 waliulizwa maswali katika kipindi Julai, 2022. Kadhalika utafiti huo umeangalia mwelekeo wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2020 na 2022 na kubaini kuwa bado hali ya uchumi ndilo malalamiko makubwa ya wananchi, ukosefu wa ajira na kipato.