Tutapigana kubakisha ndondi kwenye Olimpiki - Rais wa DBV
4 Julai 2023Rais wa shirikisho la ndondi la Ujerumani (DBV) Jens Hadler amesema kutengwa kwa shirikisho la ndondi duniani, IBA, hivi karibuni na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC, kunafanya mambo kuwa magumu zaidi lakini michezo ya Olimpiki inasalia kuwa kipaumbele cha kwanza kwa chombo chake.
"Ndondi za Olimpiki hakika ni kipaumbele kwetu kwa sababu karibu ufadhili wote unaelekezwa huko. Kama DBV, tutapigana kila mara ili kuendelea na ndondi katika Olimpiki," Hadler aliambia toleo la Jumanne la gazeti la Frankfurter Rundschau.
Soma pia: Wladimir Klitschko astaafu mchezo wa ndondi
Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC iliiondoa IBA mwezi uliopita kuhusu masuala mbalimbali kuanzia utawala na uwazi hadi ufadhili. IOC hapo awali ilikuwa imeisimamisha IBA mwaka 2019, pamoja na masuala mengine ikiwa ni pamoja na uamuzi na ujaji.
Ndondi zinaendelea kuwa kwenye mchezo ya Olimpiki, kukiwa na kikosi kazi cha IOC kinachoendesha mchezo huo 2021 mjini Tokyo na mwaka ujao mjini Paris. IOC imesema kuwa mchezo huo pia utakuwepo 2028 mjini Los Angeles.
Bodi mpya ya uongozi iliyopewa jina la World Boxing iko mbioni kuanzishwa, ikiwa na lengo kuu la kupata kutambuliwa na IOC, mchakato ambao utaihitaji kuwa na uanachama wa kutosha.
Soma pia: Bondia wa kike anasaidia jamii
IBA kuendeleza mfumo wake wa ushindani?
"Hakika itakuwa ngumu zaidi kwenye ndondi kwa sababu upande mmoja una ndondi za Olimpiki," Hadler alisema. Kwa upande wa pili, IBA iliyo na mashirikisho ya kitaifa wanachama karibu 200, huenda itaendelea kuwepo na itaendeleza mfumo wake wa ushindani, yumkini ikiwa na idadi iliyopungua ya mashirikisho ya kitaifa wanachama.
"Sasa shirikisho jipya la ulimwengu litaundwa, lakini bado kuna maswali mengi ya wazi yanayopaswa kujibiwa.
Soma pia: Mabondia Mayweather na Pacquaio wawindana
"Katika kujenga shirikisho hili jipya la dunia, kila kitu ambacho kimepelekea IBA kufika hapa ilipo sasa lazima kiepukwe tangu awali. Hii itamaanisha kazi nzuri sana, kubwa na yenye muundo.
"Moja ya maswali muhimu yatakuwa ni mashirikisho mangapi ya kitaifa yatajiunga na shirikisho jipya la dunia na ipi mipaka ya kukubalika kwa IOC katika suala hili kuhusiana na Mkataba waOlimpiki."
Hadler alisema DBV - ambayo ilikuwa na hadhi ya mwangalizi wakati World Boxing ikianzishwa, jambo lililopelekea kusimamishwa kwake na IBA - itajadili jinsi ya kuendelea katika kongamano lake baadaye mwezi huo.
Chanzo: DPAE