Tutahudhuria kuapishwa Barrow - ECOWAS
18 Desemba 2016Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ulimalizika jana (17 Disemba), ambapo viongozi wote waliohudhuria walisema watashiriki kwenye sherehe za kumuapisha rais mpya wa Gambia, Adam Barrow, hapo tarehe 19 Januari 2017.
Viongozi hao pia waliahidi "kuhakikisha usalama na ulizi wa rais mteule", ambaye amesema anahofia maisha yake.
Marais 11 waliohudhuria mkutano huo wa kilele uliofanyika Abuja, Nigeria, walikubaliana "kuchukuwa hatua zozote za lazima kuhakikisha kuheshimiwa kwa matokeo" ya uchaguzi wa Gambia yanaheshimiwa, huku wakimtolea wito Rais Jammeh, ambaye mwenyewe hakuhudhuria mkutano huo, kukubali matokeo na kutokuzuwia ukabidhianaji wa amani wa madaraka.
Mkutano huo wa kilele uliteua kamati ya upatanishi inayoongozwa na Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria akisaidiwa na Rais John Dramani Mahama wa Ghana, ambaye mwenyewe alikubali kushindwa kwenye uchaguzi uliofanyika siku chache baada ya ule wa Gambia.
Wakati huo huo, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein, ameonya kuwa hatua ya serikali ya Jammeh kusambaza wanajeshi katika maeneo yote ya Gambia kunaongeza hali ya vitisho na unyanyasaji.
"Jambo hili linatia wasiwasi sana, hasa ikizingatiwa rikosi ya uvunjwaji wa haki za binaadamu nchini Gambia, yakiwemo matumizi ya nguvu za kupindukia dhidi ya waandamanaji, uwekaji wa ovyo ovyo vizuizini na vifo wakiwa mikononi mwa polisi, na pia tuhuma za mateso na kutendewa vibaya kwa wale wanaoshikiliwa," alisema Zeid.
Hatua za kijeshi za ECOWAS
Rais Yahya Jammeh wa Gambia aliwashangaza raia wake kwa kukubali kushindwa siku moja tu baada ya uchaguzi wa tarehe 1 Disemba, na kisha kubadili kauli yake na kutaka ufanyike uchaguzi mpya wiki moja baadaye.
Kwa pamoja, Umoja wa Mataifa, Marekani na Umoja wa Afrika, wamelaani hatua hiyo.
Ukaidi wa Jammeh unaipa changamoto la kwanza jumuiya ya ECOWAS, ambayo imetumia miaka 25 kuilea demokrasia kwenye eneo ambalo lilikuwa maarufu kwa mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara.
Endapo itachukuwa hatua za kijeshi itaifanya kuwa jumuiya ya kwanza ya kikanda kukubaliana juu ya hatua ya kijeshi dhidi ya mwanachama wake anayeshukiwa kwa kuvunja haki za binaadamu na kukanyaga misingi ya kidemokrasia.
Mapema wiki hii, akizungumza na kituo cha redio cha Ufaransa, rais wa ECOWAS, Marcel de Souza, alisema wiki hii kwamba kama diplomasia itashindwa, basi uingiliaji kati kijeshi na "hatua za kukomesha" lazima zizingatiwe kwa Gambia.
Kigeugeu cha Jammeh
Wachambuzi wanasema Jammeh aliamua kubadili uamuzi wake wa awali wa kuyatambua matokeo ya kushindwa, baada ya mmoja wa maafisa wa upinzani kusema kwamba atapaswa kushitakiwa kwa uvunjaji wa haki za binaadamu.
Akitumia sababu ya makosa kwenye ujumlishaji wa matokeo, Jammeh alipuuzia tamko la Tume Huru ya Uchaguzi iliyosema kuwa bado mshindi anabakia kuwa Barrow akiwa na kura 227,708 dhidi ya 208,487 alizopata kiongozi huyo aliyekaa madarakani kwa miaka 22.
Jumanne iliyopita (13 Disemba), chama tawala kilifungua kesi mahakamani kupinga matokeo hayo, hatua ya kisheria ambayo ina utata mkubwa kutokana na ukweli kuwa Mahakama ya Juu ya Gambia haina akidi. Marekani ilisema ina mashaka "endapo ni mahakama huru inayoweza kuhakikisha mchakato wa kidemokrasia wa Gambia unaheshimiwa."
Siku hiyo hiyo, Jammeh alituma wanajeshi kuzishikilia ofisi za tume ya uchaguzi katika mji mkuu, Banjul, muda mfupi kabla ya ujumbe wa viongozi wa Afrika Magharibi kuwasili kwa mazungumzo ya kusaka suluhu.
Jammeh aliingia madarakani mwaka 1994 kwa mapinduzi yasiyo umwagaji damu, kwenye taifa hilo dogo la raia milioni 1.9, linalofahamika kwa fukwe zake za kuvutia, magharibi mwa Afrika.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Zainab Aziz