1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia yawakamata washukiwa watatu

24 Desemba 2016

Ujerumani inaendelea kuwasaka washukiwa zaidi ambao huenda walishirikiana na mtuhumiwa wa shambulizi la lori mjini Berlin ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi ya Italia

https://p.dw.com/p/2Uq4E
Italien Mailand Sicherheitskräfte vor Mailänder Dom mit Weihnachtsbaum
Picha: picture-aliance/AP Photo/L. Bruno

Wizara ya mambo ya ndani ya Tunisia imesema mmoja wa wanaume waliokamatwa ni mpwa wa mtuhumiwa wa shambulizi la Berlin Anis Amri ambaye alikuwa mzaliwa wa Tunisia. Taarifa hiyo imesema watu hao watatu, wenye umri wa kati ya miaka 18 na 27, walikamatwa Ijumaa na walikuwa wanachama wa "kikundi cha kigaidi” chenye mafungamano na gaidi Anis Amri.

Taarifa hiyo haikutaja uhusiano wowote kati ya wanaume hao watatu na shambulizi la Jumatatu, ambapo Amri anaaminika aliteka nyara lori na kulitumia kuwakayaga watu katika soko moja la Krismasi mjini Berlin, na kuwauwa watu 12. Mwanamme huyo mwenye umri wa miaka 24 alisakwa kwa siku nne kabla ya kupigwa risasi na kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa Italia baada ya yeye kufyatua risasi kwanza. Kundi la IS lilidai kuhusika na shambulizi la Berlin, ambalo lilitoa video ikimwonyesha Amri akiapa kuwa mtiifu kwa kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi

Deutschland Weihnachtsansprache Bundespräsident Gauck
Rais wa Ujerumani Gauck ametoa wito wa uvumilivuPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Wizara ya mambo ya Tunisia imesema Amri alituma hela nyumbani kwa mpwa wake na akajadiliana naye kuhusu itikadi za mapigano ya jihadi. Taarifa hiyo imesema mtoto wa kiume wa dada yake Amri alikiri kuwa na mawasiliano na mjomba wake kupitia huduma ya kutuma ujumbe wa simu ya Telegram.

Amri anadaiwa kumtaka mpwa wake kuanza kufuata itikadi kali za "takfiri” na akamtaka atangaze utiifu wake kwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS. Ukweli kwamba Amri aliweza kusafiri hadi Italia bila kuzuiwa licha ya kutolewa waranti wa kukamatwa kwake iliyotolewa Ulaya nzima umezusha maswali magumu kwa mashirika ya kijasusi.

Mashirika ya usalama Ujerumani pia yamekabiliwa na shutuma kali kwa kutomfuatilia kwa umakini Amri kabla ya shambulizi, ingawa walikuwa wanamfahamu na alishukiwa kwa kupanga shambulizi. Lakini waziri wa Mambo ya ndani, Thomas De Maiziere, amekanusha madai kuwa mfumo mzima wa usalama ulishindwa.

Kansela Merkel ameahidi kutafanywa tathmini kamili ya namna mshukiwa huyo wa kigaidi alivyoweza kukwepa mitego ya usalama.     

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusra Buwayhid