Tunisia yaadhimisha mwaka mmoja baada ya kuondoka Ben Ali
14 Januari 2012Baada ya mapinduzi hayo, ulifanyika uchaguzi wa amani mwezi wa Oktoba mwaka uliyopita. Wimbi hilo la mageuzi limechochea harakati zilizoondoa pia tawala za muda mrefu za kimabavu za Hosni Mubarak wa Misri na Muammar Gaddafi wa Libya.
Miongoni mwa wageni waalikwa mashuhuri katika hafla ya leo, ni Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika, Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani wa Qatar, mmoja kati ya wafadhili wakuu wa mageuzi katika nchi za Kiarabu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Saad-Eddine El Othmani anaemwakilisha Mfalme Mohamed wa sita. Kiongozi wa Baraza la jipya Mpito linaloongoza Libya, Mustafa Abdel Jalil anatarajiwa kuhudhuria sherehe hizo.
Maelfu wa Watunusia walisherehekea maadhimisho ya kwanza hapo Desemba 17, ikiwa ni siku ambayo, muuza matunda Mohamed Bouazizi, alijichoma moto akiwa na umri wa miaka 26. Kitendo hicho ndio kilichozusha vuguvugu la mageuzi nchini Tunisia.
Ben Ali ambae amepatikana na hatia ya uhalifu wa kiuchumi pamoja na uhalifu mwingine katika mahakama ya Tunisia, amepewa hifadhi nchini Saudi Arabia baada ya ndege yake kukataliwa kutua Ufaransa. Kwa mujibu wa serikali mpya ya Tunisia, Saudi Arabia mara mbili imekataa kuitikia maombi ya kumrejesha nyumbani Ben Ali anaekabiliwa na mashtaka mbali mbali nchini Tunisia.
Miongoni mwa changamoto zinazokabiliwa na utawala mpya wa Tunisia ni ukosefu mkubwa wa ajira. Rais wa Tunisia Moncef Marzouki leo anatarajiwa kutoa msamaha kwa wafungwa 1000.