Tunisia washerehekea miaka mitatu ya mapinduzi ya udikteta bila ya katiba mpya
14 Januari 2014Rais Moncef Marzouki, waziri mkuu anayemaliza muda wake, Ali Larayedh, na aliyemteua kuchukua nafasi yake, Mehdi Jumaa, ni miongoni mwa viongozi kadhaa wa serikali waliohudhuria uzinduzi wa sherehe hizo za kumbukumbu ya tukio la mapinduzi dhidi ya udikteta, katika kitongoji cha Kasbah kilichopo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tuni), ambako pia ni makao makuu ya serikali.
Mojawapo ya shamrashamra hizo ni maandamano yaliyopangwa na Chama cha Ennahda katika mtaa wa Habib Bourguiba, kulipokuwa kituo cha raia waliokuwa katika mgomo wa siku kadhaa wakati wanaupinga utawala wa Zine El Abidine Ben Ali, waliyefanikiwa kumng'oa madarakani hapo tarehe 14 Januari 2011, baada ya kuwa amewatawala kwa mfumo wa kidikteta kwa miongo kadhaa.
Ulinzi mkali wakati wa sherehe
Polisi walisambazwa katika kila pembe ya mji huo kulinda doria. wa ajili ya kufanya doria ya usalama wa wananchi. Licha ya hamasa waliyokuwa nayo raia katika uzinduzi wa sherehe hizo, hofu pekee iliyokuwepo ni uchelewaji wa kuidhinishwa rasmi katiba yao mpya wanayoisubiri kwa hamu, ambayo ilitarajiwa kuwa tayari wakati wa sherehe hizo, lakini mpaka sasa bado inafanyiwa kazi.
Katiba hiyo yenye vifungu 150, ambayo ni ya tatu kufanyiwa marekebisho, ilipaswa kuwa imekwishahakikiwa, baada ya mjadala wa wabunge kuhusu kuondoa baadhi ya vipengele uliochukua karibu wiki mbili, kukamilika.
Tunisia wataka raisi mwenye vigezo sahihi
Mojawapo ya vifungu vilivyopendekezwa kuwekwa ni ulazima wa kuwa na rais mwenye vigezo vinavyofaa, na uwepo wa mamlaka ya waziri mkuu. Pia wabunge wa nchi hiyo walipinga nafasi ya serikali kuteua majaji.
Raia wa Tunisia wanasubiri kuundwa kwa serikali mpya chini ya Jumaa, itakayosimamia nchi kuelekea uchaguzi mpya.
Uteuzi wa Jumaa wiki iliyopita, ulifanyika baada ya makubaliano ya kumaliza mvutano wa kisiasa kwa mwezi mzima, na kufuatiwa na maamuzi ya kuondoka madarakani kwa uongozi wa chama cha Kiislamu cha Ennahda, klichoshinda kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia baada ya mapinduzi ya umma dhidi ya dikteta Ben Ali.
Katika hotuba yake ya jana, Rais Marzouki alikiri kuwa viongozi wa serikali hawakuweza kukidhi matumaini makubwa ya kimageuzi waliyonayo wananchi miaka mitatu ya mapinduzi baada ya mapinduzi.
Mwandishi: Diana kago/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef