1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia: Miaka miwili baada ya mapinduzi

14 Januari 2013

Tunisia ilianzisha vugugvugu la mapinduzi yaliyokuja kusambaa katika ulimwengu mzima wa Kiarabu. Lakini ni raia wachache tu wa nchi hiyo wanaojisikia kusherehekea kwani demokrasia bado haijawafikia wote.

https://p.dw.com/p/17JPd
Watunisia wakiadhimisha siku ya mapinduzi
Watunisia wakiadhimisha siku ya mapinduziPicha: DW

Miaka miwili iliyopita, siku kama ya leo Zine El Abidine Ben Ali, aliyekuwa rais wa Tunisia, aling'olewa madarakani. Alikuwa ameiongoza nchi yake kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miaka 20. Lakini njia ya kuelekea kupata demokrasia ya kweli inaelekea kuwa ngumu kuliko raia wengi wa Tunisia walivyodhania. Mohamed ni mwanafunzi katika nchi hiyo. Anaelezea kwamba mwanzoni mwa mwaka 2011 raia wa Tunisia waliandamana kudai uhuru na usawa lakini mpaka sasa hakuna mabadiliko yaliyotokea: "Hali ingeweza kuwa nzuri zaidi. Kuna matatizo mengi sana ya kijamii na hata ya kisiasa kutoka upande wa serikali na wa upinzani. Kama wangefanya kazi kwa ushirikiano, tungeweza kusonga mbele."

Uchumi wa Tunisia umeathiriwa na matokeo ya mapinduzi. Watalii wengi wanaogopa kuitembelea nchi hiyo wakihofia kutokea kwa machafuko. Hata wawekezaji kutoka nje wamekuwa waangalifu zaidi kwa sababu mara kwa mara pametokea migomo ya wafanyakazi inayosimamisha kazi viwandani.

Rais wa zamani wa Tunisia, Ben Ali
Rais wa zamani wa Tunisia, Ben AliPicha: picture-alliance/dpa

Ukosefu wa ajira bado tatizo

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, asilimia 17 ya raia wa Tunisia hawana ajira. Idadi hii ni kubwa zaidi ya ile iliyokuwepo kabla ya mapinduzi. Katika baadhi ya maeneo yaliyopo katikati ya nchi, zaid ya nusu ya wakaazi hawana ajira. Watunisia wanaona wazi wazi athari za mapinduzi katika maisha yao ya kila siku: Bei za vyakula zimepanda kwa kasi, kwa miezi mitatu sasa hapakuwa na maziwa yaliyouzwa. Vyakula kama nyama na viazi vimepanda bei kiasi kwamba watu wengi wanashindwa kabisa kuvinunua.

Mwanasheria Hayat Jazar ni mmoja wa watu waliofika kuandamana na kutoa hasira yao: "Hakuna kinachoendelea. Hakuna haki na hakuna ajira. Matakwa ya raia hayakutekelezwa, zaidi ya haki ya kutoa maoni," anasema Hayat. "Serikali chini ya chama cha Ennahdha inafanya kila juhudi kutufumba midomo. Hivi karibuni tutakuwa na utawala kama ule wa Ben Ali."

Raia wa Tunisia bado wana matumaini
Raia wa Tunisia bado wana matumainiPicha: picture-alliance/dpa

Waandamanaji hawa walikuwa wamedai katiba mpya ili kuachana kabisa na mifumo ya kizamani na ya kidikteta. Mwezi Oktoba mwaka 2011, kwa mara ya kwanza Watunisia walichagua baraza la kutunga katiba itakayoipa nchi sheria mpya. Lakini mpaka sasa, baraza hilo halijamaliza kazi ya kuandaa katiba. Hata hivyo, raia wa Tunisia hawakati tamaa na wanaamini kwamba ipo siku watapata mabadiliko waliyoyatazamia wakati wa mapinduzi ya kumwangusha Ben Ali.

Mwandishi: Sarah Mersch

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf