Tunisia kuunda kamati ya kuandika katiba mpya
2 Mei 2022Rais wa Tunisia Kais Saied amesema serikali yake itaunda kamati ya kuandika katiba mpya ya kile alichokiita "Jamhuri Mpya" nchini Tunisia. Saied ameyasema haya kupitia hotuba iliyorushwa na televisheni ya taifa nchini humo. Amesema kamati hiyo itakamilisha majukumu yake katika kipindi cha siku chache zinazokuja.
Kiongozi huyo amearifu kuwa mazungumzo ya kitaifa kuhusiana na mageuzi hayo yatajumuisha mashirika makuu 4 nchini Tunisia ya chama cha wafanyakazi, muungano wa wanasheria, shirikisho la viwanda na biashara na shirika la haki za binadamu la Tunisia.
Hivi karibuni Saied alijipa nguvu ya kumteua mkuu wa tume ya uchaguzi, hatua ambayo wakosoaji wanasema inalenga kuidhoofisha tume hiyo kuelekea kura ya maoni kuhusu katiba ambayo ilikuwa imepangiwa kufanyika mwezi Julai na uchaguzi wa wabunge wa mwezi Desemba.