Tunisia kidedea , Cape Verde na Congo sare
23 Januari 2015Tai wa Carthage Tunisia , wanaongoza kwa point mbili zaidi ya timu inayofuatia wakati ukibakia mchezo mmoja baada ya kunyakua ushindi wa mabao 2-1 kutoka kwa Zambia Chipolopolo ambao wamepoteza nafasi kadhaa za wazi katika uwanja wa Nuevo Estadio de Ebebiyin.
Nahodha Yassine Chikhaoui alitumbukiza wavuni bao la ushindi kwa kichwa katika dakika ya 89 baada ya Emmanuel Mayuka kuipatia Zambia bao la kuongoza katika kipindi cha pili na Ahmed Akaichi akasawazisha.
Akaichi , ambaye aliongezwa kikosini dakika za mwisho baada ya mchezaji mmoja katika kikosi hicho kuwa majeruhi, amekuwa mchezaji wa kwanza katika mashindano hayo kupachika mabao mawili.
Ushindi huo ulikuwa ni faraja kubwa kwa Tunisia , ambao walikula chakula cha usiku kwa kutumia mishumaa na kulala wanne katika chumba kimoja baada ya sehemu ya hoteli yao kujaa maji.
Sare chapwaa
Iwapo mchezo wa kwanza ulistahili mashabiki kulipa fedha za kiingilio , mashabiki hao walifadhaishwa na sare ya bila kufungana kati ya Cape Verde na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.
Ni mchezo uliokuwa hauna nafasi za wazi za kufunga mabao ukishindana na sare ya bila kufungana kati ya wenyeji Guinea ya Ikweta na Burkina Faso saa 24 zilizopita kwa sare yenye kuchosha katika mashindano hayo yenye msisimko mkubwa.
Ushindi kwa Tunisia umewaweka mabingwa hao wa mwaka 2004 katika uongozi wa kundi B wakiwa na pointi nne wakati Cape Verde na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo zina pointi mbili kila moja pamoja na tofauti sawa ya magoli.
Na pamoja na kwamba mabingwa wa mwaka 2012 Zambia iko mwisho wa msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi moja, bado wananafasi katika kundi hilo pia ya kufika katika awamu ya mtoano ya timu nane.
Chipolopolo inabakia mjini Ebebiyin kuikabili Cape Verde siku ya Jumatatu wakati Tunisia na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo zitaoneshana kazi mjini Bata wakati mmoja.
Kocha bado haamini timu yake
Licha ya ushindi kocha wa Tunisia George Leekens ameendelea kutojigamba kwa kikosi chake baada ya kusisitiza kabla ya mchezo wa jana kuwa hawamo katika orodha ya vigogo vinavyoweza kutoroka na taji hilo.
Kocha wa Zambia Honour Janza pia nae hakufurahishwa na matokeo wakati Zambia imekwenda michezo sita ya kombe la mataifa ya Afrika bila ushindi katika muda wa miaka minne.
Leo jioni(23.01.2015) itaingia uwanjani Ghana ikipambana na Algeria na baadaye itakuwa zamu ya Afrika kusini , Bafana bafana ikiumana na Senegal.
Wakati huo huo shirikisho la kandanda barani Afrika CAF limethibitisha jana Alhamis kuwa michuano ya kuwania kufuzu kucheza katika kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi itaanza Oktoba mwaka huu, wakati safari ya kuelekea katika kinyang'anyiro kingine cha kombe la mataifa ya Afrika itaanza rasmi Juni mwaka huu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre