1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tundu Lissu arejea Tanzania

Admin.WagnerD27 Julai 2020

Kiongozi wa chama upinzani nchini Tanzania Chadema, Tundu Lissu ametimiza ahadi yake kwa kurejea nyumbani na kupata mapokezi makubwa licha ya onyo lililotolewa na jeshi la polisi kupiga marufuku mikusanyiko yoyote.

https://p.dw.com/p/3fzyj
Tundu Lissu in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Lissu aliyetangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwezi Oktoba alitua katika ardhi ya Tanzania saa 6:23 na kupokelewa na viongozi wenzake kabla ya baadaye kujitokeza katika umati mkubwa wa watu uliofurika katika uwanja wa taifa wa mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kumlaki

Ingawa kulikuwa na onyo la jeshi la polisi lilitaka kutowepo kwa mikusanyiko yoyote ya watu wakati wa ujio wa mwanasiasa huyo anayetajwa kuwa na uwezo wa kusubutu kusema hadharani pasina woga, wafuasi na wanachama wa chama hicho, halionyesha furaha yao na kumiminika kwa wingi uwanjani.

Viongozi mbalimbali, kuanzia wale wa kikanda, kitaifa pamoja na wabunge waliomaliza muda wao walikuwa sehemu ya umati huo wakiwa katika sare maarufu ya chama hicho yaani mavazi aiana ya kombati wengine wakiwa wamevalia fulani zenye ujumbe uliomtaja mwanasiasa huyo.

Tundu Lissu und Harrison Mwilima
Tundu Lissu alipozungumza na mwakilishi wa DW-Kiswahili huko jijini Berlin, Harrison MwilimaPicha: DW/M. Fischer

Baadhi ya wabunge waliozungumza na idhaa hii muda mchache baada ya Lissu kutua nchini, akiwa mbunge aliyemaliza muda wake, Joseph Mbilinyi walisema kuwa chama chao sasa kinaweka gia mpya uitakayoleta furaha katika siku za usoni.

Wengi walikuwepo uwanjani hao walionekana kushindwa kujizua kutokana na furaha waliokuwa nayo huku kukishuhudiwa vituo vya hapa na pale kama vile baadhi yao kupoteza viatu hali iliyowafanya kutembea pekekupeku huku wakiendelea kumshangilia kiongozi wao.

Lissu aliondoka uanjani hapo na kusindikizwa na msafara wa magari na watembea kwa miguu walioambatana naye hadi makao makuu ya chama hicho eneo la Kinondoni. Jeshi la polisi mara hii walijiweka kando kuingilia msafara huo, licha ya marufuku yao walioyoitoa mwishoni mwa wiki.

Mwanasiasa huyo anarejea nchini tayari kwa ajili ya kujiunga katika mchaka mchaka wa kuelekea uchaguzi mkuu ambao umetangazwa kufanyika siku ya Jumatano ya tarehe 28, Oktoba. Lissu alinusurika katika jaribio la mauwaji lililotokea Septemba 27, 2017 wakati akirejea nyumbani kwake baada ya kuhudhuria vikao vya bunge.