1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia: Tumuenzi baba wa taifa kwa kupinga ufisadi

Saleh Mwanamilongo
14 Oktoba 2022

Leo ni kumbukumbu ya miaka 23 tangu kifo cha Mwalimu Julius Kambarange Nyerere anayetambuliwa nchini Tanzania kama baba wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4IBs1
Mwalimu Nyerere na Leoporld Sedar Senghor, Rais wa Zamani wa Senegal
Mwalimu Nyerere na Leoporld Sedar Senghor, Rais wa Zamani wa SenegalPicha: Getty Images/AFP

Shughuli nyingine inayofanyika hii leo pamoja na kumbukumbu hiyo ya kifo cha Mwalimu Nyerere ni kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na wiki ya vijana kitaifa. Shughuli zote hizo zinafanyika katika uwanja wa Bukoba mkoani Kagera ambapo mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hotoba yake ya kumkaribisha rais, makamo wa Rais Philip Mpango amesema kama ilivyo kwa mataifa mengine, Tanzania inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi. Amesema changamoto hiyo kubwa kwa hivyo kila taifa lina wajibu kwa hivyo ametaka miradi ya mazingira, sasa ikaguliwe kila wilaya kuanzia mwaka ujao wa fedha.

''Tunao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba tumewachia watoto wetu hawa tunaowajibu wa kuwaachia Tanzania nzuri,Tanzania inayopendeza na vijito vingi vya maji na bahari nzuri na maziwa mazuri.'' alisema Mpango.

''Kuuenzi umoja na mshikamano''

Rais Samia awataka Watanzania kupambana na ufisadi
Rais Samia awataka Watanzania kupambana na ufisadiPicha: Boniface Muthoni/ZUMA Wire/IMAGO

Mgeni rasmi wa hafla hiyo rais Samia Suluhu amewataka watanzania kuendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuendelea na vita dhidi ya rushwa na ufisadi.

''Nami nitumie fursa hii kuwaomba Watanzania wote kuendeleza kuwaenzi wazee wetu hawa,kumuenzi baba wa taifa, kwa kupinga vitendo vya ufisadi, rushwa, chuki, dharau. Kuuenzi umoja na mshikamano.'', alisema Samia.

Julius Kambarage Nyerere, anafahamika zaidi kwa jina la Mwalimu kutokana na taaluma yake ya zamani kabla ya kujiunga na harakati za ukombozi. Aliiongoza Tanganyika kutoka mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi ilipojiunga na Zanzibar kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964 na kisha kuendelea kuwa rais wa jamhuri hiyo mpya hadi alipoondoka mwenyewe madarakani mwaka 1985. Alifariki dunia tarehe 14 Oktoba 1999 wakati akipatiwa matibabu mjini London nchini Uingereza.