1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Kenya yaahirisha uchaguzi katika majimbo 4

Shisia Wasilwa26 Oktoba 2017

Uchaguzi utarudiwa tarehe 28 mwezi huu katika Maeneo manne kutokana na machafuko ambayo yalitokea. Mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi amesema kaunti zilizoathirika ni Siaya, Migori, Kisumu na Homa Bay

https://p.dw.com/p/2mZU0
Afrika - Polizei patroulliert in Kibera Slums in Neirobi Kenia
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Bandic

Uchaguzi utarudiwa tarehe 28 mwezi huu katika Maeneo manne katika maeneo ya Nyanza kutokana na machafuko ambayo yalitokea. Mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi Wafula Chebukati amesema kuwa kaunti zilizoathirika ni pamoja na Siaya, Migori, Kisumu na Homa Bay ambazo ni ngome za upinzani. Hata hivyo uchaguzi wenyewe umeligawanya taifa katika makundi mawili ya wale wanaounga serikali na wanaoupinga. Rais Kenyatta amesema kuwa kuna uwezekano wa kufanya mazungumzo na upande wa upinzani.

Vituo 40,800 vya kupiga kura kote nchini vimefungwa baada ya Tume ya Kusimamia Uchaguzi kufunga kazi leo, huku Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kushinda kwenye uchaguzi mpya wa rais ulioitishwa na mahakama ya Juu, baada ya ule wa kwanza kubatilishwa kwa kutozingatia sheria na katiba.

Sasa ni bayana kuwa uchaguzi utarudiwa katika baadhi ya maeneo ya Nyanza kama alivyosema mwenyekiti wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi, Wafula Chebukati. "Homa Bay, Kisumu, Migori na Siaya Uchaguzi umeahirishwa hadi Jumamosi tarehe 28 juma hili mwaka 2017."

Watu wapiga foleni kupiga kura naye afisa wa polisi aliyejihami kwa bunduki akishika doria mjini Nairobi Kenya
Watu wapiga foleni kupiga kura naye afisa wa polisi aliyejihami kwa bunduki akishika doria mjini Nairobi KenyaPicha: picture-alliance/AP Photo/S.Abdul Azim

Wapiga kura wachache wajitokeza

Katika kitovu cha nchi, jijini Nairobi, vituo vilivyofunguliwa mchana havikuwa na foleni ndefu huku wapiga kura wachache wakijitokeza kupiga kura. Maduka mengi na biashara nyingi zilifungwa baada ya serikali kutenga siku hii kuwa ya mapumziko. Hata hivyo wachache waliojitokeza kupiga kura walikuwa na rai moja. Amani.

Naibu rais William Ruto alipiga kura katika jimbo lake la Uasin Gishu ambayo ni moja ya ngome za chama cha Jubilee. Ameelezea imani yake kuhusu hatua hiyo aliyosema ni haki ya kila mkenya kutekeleza. Alipuuzilia mbali hatua ya upinzani kutoshiriki kwenye marudio ya uchaguzi huo. Ruto ameongeza kuwa "Mimi nimefurahi kupata nafasi kama mkenya, nafasi ya kipkee kupiga kura kwa njia huru na kidemokrasia tukiwa na malengo tunatimiza malengo ya katiba yetu ya Kenya."

Wito wa mazungumzo kati ya Rais Kenyatta na Raila odinga

Watu wakipiga kura katika eneo la uwakilishi la Gatundu
Watu wakipiga kura katika eneo la uwakilishi la GatunduPicha: Reuters/S. Modola

Wakenya wengi wanahisi kuwa viongozi wakuu, Rais Kenyatta na Raila Odinga wanastahili kuketi kwenye meza ya mazungumzo ili kukwamua taifa kwenye lindi ambalo limesakama taifa. Huku rais Kenyatta akisema kuna uwezekano wa mazungumzo baina yake, upande wa upinzani umefunga milango hiyo na sasa umebuni vugu vugu linalolenga kupigania haki zao.

Rais Kenyatta anafahamu uzito unaomkodolea macho wa kuliunganisha taifa. Kenyatta ameongeza kusema "Ni wajibu wa yeyote atakayechaguliwa kuwa rais, kuleta utangamano na umoja, na iwapo wakenya watanichagua huo ni wajibu wangu hilo ni jukumu langu na nina nuia kulitekeleza." 

Uchaguzi wa leo ni wa kihistoria kwani, ni mara ya kwanza barani Afrika na ya tatu ulimwenguni kwa taifa lolote kubatilisha matokeo ya urais na kuandaa tena mwingine, lakini je uchaguzi huo umeafiki viwango vinavyohitajika?

 

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi