1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Uchaguzi Afghanistan kuamua karibuni juu ya madai ya udanganyifu.

12 Oktoba 2009

Waangalizi wa kimataifa wasema udanganyifu ulikua mkubwa mno.

https://p.dw.com/p/K4OB
Masanduku ya kura yakisubiri kuhesabiwa upya.Picha: AP

Tume ya Uchaguzi nchini Afghanistan inatarajia kutangaza mnamo siku chache zijazo uamuzi wake juu ya madai ya Udanganyifu wakati wa uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo.

Maafisa nchini humo wamesema kuwa uamuzi huo unaweza kutangazwa kabla ya mwisho wa wiki juu ya nani atakuwa Rais ajaye wa nchi au kama kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi kwa wagombea wakubwa wawili, Rais anayetetea nafasi yake Hamid Karzai na mpinzani wake mkuu, Abdullah Abdullah.

Wa Afghan walipiga kura Agosti 20 mwaka huu, kuchagua rais wa nchi hiyo, lakini uchaguzi huo ulitawaliwa na madai na madai ya kufanyika kwa udanganyifu, ambayo mengi yalimkabili Rais Hamid Karzai, ikiwemo uchunguzi uliofanywa na Wangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya kutilia shaka robo ya kura zote au kura milioni 1.5 zilizopigwa.

Wakati maafisa nchini Afghanistan wakitangaza hayo, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Kai Eide amekiri kwamba Uchaguzi huo wa Rais wa mwezi Agosti, ulikuwa na udanganyifu mkubwa,'' ilikuwa ikidaiwa kwamba kulikuwa na udanyanyifu kwa asilimia 30, hakuna njia ya kujua kwa hatua hiyo, ni kiwango gani cha udanganyifu kipo."

Sijui, hakuna anayejua.Naweza kusema tu kwamba kulikuwa na udanganyifu mkubwa. Taarifa zozote kamili kwa kipindi hiki zitakuwa hakika ni za kukisia.

Kwa hivyo sitataja idadi kamili...''

Ameyasema hayo jana katika mkutano wake na Waandishi wa Habari kujibu tuhuma zilizotolewa na msaidizi wake wa zamani Peter Galbraith kwamba alificha ushahidi wa vitendo vya udanganyifu katika uchaguzi huo, katika hali ya kumkingia njia ya ushindi Rais Karzai.

Peter Galbraith Afisa mwandamizi wa Marekani katika ubalozi wa umoja wa mataifa alipoteza kazi yake baada ya kuhitilafiana na viongozi wake kuhusiana na jinsi ya kulishughulikia suala la madai makubwa ya udanganyifu katika uchaguzi mkuu.

Bwana Karzai ameongoza katika matokeo ya wali ya uchaguzi huo kwa kupata asilimia 55 ya kura, huku mpinzani wake Abdullah Abdullah akipata karibu asilimia 28.

Maandalizi yamekuwa yakifanywa kwa ajili ya kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi kati ya Rais Karzai na mpinzani wake huyo, ambapo wachambuzi wa mambo wanasema inapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo kabla ya kuanza majira ya baridi, hali ambayo italeta ugumu wa kuyafikia maeneo mengi ya nchi hiyo.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri:Sekione Kitojo