1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsunami katika mfumo wa fedha wa kimataifa

Othman, Miraji23 Septemba 2008

Mzozo mkubwa katika mfumo wa kifedha wa kimataifa

https://p.dw.com/p/FNEK
Waziri wa fedha wa Marekani, Henry PaulsonPicha: AP

Wiki iliopita ilikuwa patashikandani ya mfumo wa mabenki na wa taasisi za fedha za kimataifa, na yote ilitokana na mtafaruko uliotokea katika taasisi za fedha na mabenki makubwa ya huko Marekani. Hali hiyo ilihitaji idhibitiwe kwa haraka, kwani Marekani, ilivokuwa ndio muhimili mkubwa wa uchumi wa dunia, inaposhikwa na mafua, kiuchumi, basi sehemu nyingine za dunia zinapata homa, tena kali. Ili kuununsuru uchumi usikaribie kusambaratika, serekali ya Rais Bush huko Marekani ililitaka bunge liiruhusu itumie dola bilioni 700 na pia kuwa na mamlaka makubwa ya ya kujiingiza katika masuala ya uchumi, jambo ambalo halijawahi kutokea hapo kabla. Mpango huo unataka serekali iunde benki yake ya uwekezaji ili inunue mabilioni ya mikopo ya watu waliochukuwa kutoka mabenki na kununulia majumba. Fedha hizo zinazotakiwa na serekali ni asilimia tano ya mapato ya ndani ya Marekani, na karibu mara mbili ya bajeti ya serekali ya Ujerumani. Lakini zaidi ni kwamba mamlaka ambayo serekali inataka iwe nayo ni makubwa mno kwamba hayawezi kuingiliwa kati na mahakama yeyote au taasisi ya kiutawala. Na pale bunge litakapolikubalia ombi hilo, basi serekali itakopa dola hizo bilioni 700 na haitaingiliwa kati na bunge juu ya namna itakavozitumia.


Bila ya shaka, pendekezo hili la serekali ya Rais Bush litakabiliana na upinzani wa Chama cha Democratic na hasa bunge ambalo linadhibitiwa na chama hicho. Mabishano juu ya suala hili yatachukuwa sura kali zaidi kwani miezi miwili kutoka sasa Wamarekani watatakiwa wapige kura. Kuna hatari kwamba masoko ya fedha yatayumbayumba pindi mpango huu utacheleweshwa kutimizwa. Tsunami hii iliotokea katika masoko ya fedha ya Mareka, bila ya shaka, itaacha alama zake katika uchaguzi wa Novemba. Na dalili ni matamshi kwanza ya mgombea wa Chama cha Republican, John McCain:

"Seneta Obama hana mpango wake mwenyewe kukabiliana na mzozo huu wa fedha. Lazima aoneshe sasa hatua anazotaka kuchukuwa."

Naye Barack Obama wa Chama cha Democratic aliulaumu mpango huo wa George Bush, akisema kuyasaidia mabenki peke yake hakutoshi. Ni tuu kuupiga jeki uchumi wote kunakoweza kuwasidia watu wa chini. Pia kanuni za kudhibiti biashara lazima zichunguzwe:


" Mwishowe ni suala la nafasi zenu za kazi, akiba zenu katika mabenki, nyumba zenu. Vyama vyote lazima sasa vishirikiane ili kuukiuka mzozo huu."

Spika wa baraza la wawakilishi huko Marekani, Bibi Nancy Pelosi wa kutoka Chama cha Democratic, aliweka wazi kwamba wao hawako tayari kuachana na mpango wao wa kuupanua mpango huo ili kuingiza kutolewa misaada kwa wenye mikopo ya majumba pamoja na wengine, na pia, angalau, kuweka sheria za kuzuwia kutokea tena mzozo katika mabenki ya Marekani, kama ulivoonekana karibuni.

Na kuna wabunge wengine wanaosema kutaifisha mikopo mibaya ya nyumba sio jibu.

Akiupendekeza mpangi huu, waziri wa uchumi wa Marekani, Henry Paulson, alisema hiyo ni hatua ya kijasiri ya kuumaliza mzozo huu uliodumu mwaka mzima na ambao umeyazamisha mashirika makubwa kabisa ya kifedha, hivyo kuzusha michafuko katika taasisi za fedha, bei za hisa huko Marekani kuwenda chini na uchumi unaojikokota kukaribia kukwama.

"Kile tunachopendekeza ni kwamba serekali inunuwe mali zizokuwa fedha taslimu kwa kiwango kikubwa mabenki na mashirika, Hizo ndizo zinazokwamisha mfumo wa fedha."

Mzozo huu wa kifedha wa Marekani ulipata makali pale serekali ilipokataa kuiokoa benki kubwa ya Lehman Brothers. Masoko ya mikopo yalirejea nyuma kutaka kuinusuru benki hiyo isifilisike. Tena kukaenea habari kwamba kampuni kubwa kabisa la bima la huko Marekani, American International Group, AIG, lilikuwa linakabiliana na shida ya kuwalipa wateja wake na kutimiza majukumu yake mengine. Hali hiyo ilipelekea masoko ya hisa za makampuni huko kupata hasara ya asilimia 4.4, hasara kubwa kabisa kuwahi kupatikana tangu kutokea yale mashambuluio ya kigaidi ya Septemba 11 huko Marekani. Karibu ya hisa zenye thamani ya dola bilioni 700 zilipotea katika siku moja tu ya biashara.

Hali hiyo ya kufa kampuni moja na kuuzwa jingine katika Barabara ya Wall Street huko New York ilisasbabisha thamani ya dola ya Marekani kwenda chini, na pia kuishusha bei ya mafuta yasiosafishwa kufikia kwa mara ya kwanza chini ya dola mia moja kwa pipa tangu Februari 15 mwaka huu.

Mtikisiko huu mkubwa katika taasisi za mabenki na fedha huko Marekani ulianzia pale bei za majumba zilipoporomoka na kusambaa katika makampuni ambayo dhamana za mikopi yao imefungamana na mikopo ya majumba. Mara mbili mwaka jana wakuu wa serekali waliingilia kati kuyazuwia makampuni ya fedha na kuzuwia kusambaratika zaidi masoko ya nyumba. Lakini mara hii, serekali ilikaza kamba na kuiambia benki ya Lehman Brothers kwamba katu fedha za walipa kodi wa Kimarekani hazitatumiwa kuinusuru benki hiyo isifilisike.

Lakini mwanauchumni Suleiman Salim wa huko London ana maoni mengine kuhusu kuzuka kwa mzozo huuwa kifedha duniani:

Uamuzi wa Rais George Bush wa kuyapiga jeki masoko ya fedha ya nchi yake ni mabadiliko katika mtizamo wake wa kinadharia. Hivi ndivyo wanavoona baadhi ya wachunguzi wa mambo. Lakini mwenyewe, akiwahutubia Wamarekani kupitia televisheni, alikiri kwa kusema hivi:

"Huu ni mpango mkubwa kwa sababu tatizo lililoko ni kubwa, na nyinyi mnajuwa: Nitaawaambia raia wetu na kuendelea kuwakumbusha kwamba hatari ya kutofanya kitu ni kubw azaidi kuliko hatari ya matokeo ya mpangi huu, na baada ya muda tutaweza kuzirejesha nyingi ya fedha hizo."

Hatua yake hiyo inaonekana kuwa ni ya kuachana na nadharia yake kutokana na hali ya kwenda chini uchumi duniani. Mfumo wa masoko huru unajengeka na ile imani kwamba serekali inabidi ijiingitze tu katika masoko tu pale inapokuwa ni lazima.

Mwanauchumi Suleiman Salim wa mjini London anashangazwa na hatua hii ya watawala wa Marekani:

Mwenyewe Bush aliwaambia waandishi wa habari kwamba kutokana na hali tete ya masoko ya fedha ilivyo sasa, na umuhimu wa masoko hayo kwa maisha ya kila siku ya Wamarekani, ujiingizaji wa serekali sio tu ni jambo linalohitajika, lakini ni muhimu.