1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na sheria mpya za mabadiliko ya hali ya hewa

Sylvia Mwehozi
29 Machi 2017

Rais Donald Trump wa Marekani siku ya Jumanne (28.03.2017) ametia saini amri ya kubatilisha sheria zilizowekwa na rais aliyemtangulia Barack Obama za kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/2aDEN
USA Donald Trump unterzeichnet Dekret gegen Obamas Umweltspolitik
Picha: Reuters/C. Barria

Pamoja na hatua hiyo Trump, amebakisha ahadi yake wakati wa kampeni ya kuunga mkono sekta ya makaa ya mawe na kuibua maswali juu ya uungwaji mkono wa Marekani katika mkataba wa kimataifa wa kupambana na ongezeko la joto duniani. 

Akiwa amezungukwa na wachimba makaa ya mawe na wakurugenzi wa makampuni hayo, Trump alitangaza mpango wake wa "uhuru wa nishati" katika makao makuu ya shirika la kulinda mazingira.

Hoja yake ilipata upinzani kutoka kwa muungano wa majimbo 23 na serikali za mitaa pamoja na makundi ya wanaharakati wa mazingira ambao wanasema amri hiyo ni kitisho kwa afya ya jamii na kuapa kupambana mahakamani.

Amri hiyo inaulenga mpango wa nishati safi wa rais mstaafu Barack Obama, ambao uliyataka majimbo kukata uzalishaji wa kaboni kutoka katika mitambo ya kuzalisha umeme ikiwa ni kigezo muhimu katika uwezo wa taifa wa kutekeleza ahadi zake chini ya mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi uliofikiwa karibu na nchi 200 jijini Paris mwaka 2015.

Symbolbild Kohleabbau in Pakistan
Wafanyakazi wa Afghanistan wakijaza makaa ya mawe kwenye gariPicha: Getty Images/AFP/J. Eisele

Amri hiyo pia inaondoa marufuku ya utafiti na uchimbaji wa makaa ya mawe katika ardhi ya shirikisho chini ya kanuni za kupambana na uzalishaji wa methani kutoka katika uzalishaji wa gesi na mafuta na kupunguza uzito wa mabadiliko ya tabia nchi na uzalishaji wa kaboni katika sera na maamuzi ya miundombinu.

Trump amesema "utawala wangu unakomesha vita dhidi ya makaa ya mawe, tutakuwa na makaa ya mawe safi, namaanisha safi kweli. Pamoja na hatua hii ya leo, ninaweka historia ya kuondoa vikwazo katika nishati ya Marekani, kubadili  serikali kuingilia na kufuta kanuni zinazoua ajira," alisema Trump.

Wanaharakati wa nishati na wakurugenzi hata hivyo wanahoji ikiwa hatua hizo zitaathiri viwanda vyao na wanamazingira wameuita uamuzi huo kuwa ni wa kizembe.

Makundi ya kimazingira yanapinga amri hiyo yakidai kwamba ni hatari na inakwenda kinyume na mwenendo wa sasa wa kidunia ambao unaelekea katika teknolojia za nishati safi.

Bildergalerie Klima Proteste Grossbritannien Bristol
Waandamanaji nchini Uingereza wakitaka hatua kuchukuliwa dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchiPicha: imago/Xinhua

Katika taarifa yao, muungano wa majimbo mengi yakiongozwa na wademocratic na serikali za mitaa wanasema kwamba hawatasita kuwalinda wale wanaowatumikia, ikiwemo kupinga vikali mahakamani vitendo vya rais Trump vya kupuuza sheria na umuhimu wa kufichua tishio halisi la mabadiliko ya hali ya hewa.

Marais wa Marekani wamekuwa wakilenga kupunguza utegemezi wa mafuta ya kigeni tangu kuwekwa kwa vikwazo vya mafuta kwa nchi za kiarabu mwaka 1970, na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta. Lakini bado nchi hiyo inaagiza kiasi cha mapipa milioni 7.9 ya mafuta machafu ama yasiyosafishwa, kiasi kinachotosheleza mahitaji ya mafuta nchini Japan na India kwa pamoja.

Wanasayansi wengi wanaamini kwamba matumizi ya binadamu ya mafuta na makaa ya mawe kwa ajili ya nishati ni chanzo kikubwa cha mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha maafa kadhaa yakiwemo ukame na vimbunga vya mara kwa mara.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba