Trump na Kim wakutana katika mazungumzo ya kihistoria
12 Juni 2018Trump alikuwa wa kwanza kuwasili kwenye hotel hiyo saa mbili na dakika chache muda wa Singapore, akifuatiwa na Kim, aliyeingia na msafara wa magari yapatayo 20.
Kulingana na ratiba ya mazungumzo hayo, Trump na Kim wamekutana peke yao kwenye meza ya mazungumzo, wakisindikizwa tu na wakalimani wao. Baadaye ilitarajiwa kwamba maafisa wa pande zote wangejiunga na mkutano huo, katika mazungumzo ambayo yataendelea hadi wakati wa chakula cha mchana. Inatarajiwa kwamba baada ya mazungumzo hayo Rais Trump atazungumza na waandishi wa habari, na kisha kupanda ndege na kuondoka kurudi mjini Washington.
Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo ya kihistoria Trump alionekana mwenye matumaini. Kupitia mtandao wake wa Twitter amesema mkutano huo, wa kwanza kabisa kati ya kiongozi wa Korea Kaskazini na Rais wa Marekani aliyeko madarakani, ungekuwa na matokeo ya kufurahisha kwa Korea Kaskazini na kwa dunia nzima.
Trump awakejeli wakosoaji
Lakini pia hakukosa vijembe kwa wakosoaji wake, ''Wenye chuki na walioshindwa wanasema hali ya kwamba nimekuja katika mkutano huu ni hasara kwa Marekani'', alidhihaki Trump kupitia ukurasa wake wa twitter.
Aliendeleza mashambulizi akisema wachambuzi hawana kingine cha kusema, licha ya kwamba amefanikiwa kuwakomboa raia wa Marekani waliokuwa wakishikiliwa nchinin Korea Kaskazini.
Hakuna mengi yanayojulikana kuhusu mazungumzo hayo hadi pale taarifa itakapotolewa baadaye, lakini waziri wa mabo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo, akizungumza jana mjini Singapore amesema Marekani haitaridhishwa na chochote mbali na kuondolewa kikamilifu kwa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea, ambako kunathibitishwa na ukaguzi, kwamba ni hatua isiyoweza kurudi nyuma.
Matokeo kamili kujulikana baadaye
Kitu kingine ambacho bado hakijulikani ni muundo wa makubaliano ya kutimiza azma hiyo ya kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea, yakiwepo mashaka juu ya iwapo Korea Kaskazini itaridhia kuachana na mpango wake wa silaha hizo kwa kiwango ambacho kinatakiwa na Marekani, bila hakikisho la usalama wake wa baadaye.
Trump na Kim waliwasili mjini Singapore Jumamosi, na wote kwa nyakati tofauti wamekutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo mwenyeji Lee Hsien Loong. Vile vile maafisa waandamizi wa Marekani na wenzao wa Korea Kaskazini wamefanya mazungumzo ya faragha kabla ya mkutano wa kilele wa leo jumanne.
Mkutano wa ana kwa ana baina ya Donald Trump na Kim Jong-un haukuwa kitu kinachofikirika miezi michache iliyopita, wakati viongozi hao walipokuwa wakibadilishana matusi na kutishiana kwa silaha za nyuklia.
Ingawa vita vya Korea vilimalizika mwaka 1953, vita kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini inayoungwa mkono na Marekani bado havijamalizika rasmi, kwa sababu ingawa makubaliano yalifikiwa kusitisha mapigano, pamde hizo bado hazijasaini mkataba wa amani.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, rtre
Mhariri: Caro Robi