1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump, May kujadili mahusiano ya nchi zao

Sylvia Mwehozi
27 Januari 2017

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, anatarajiwa kukutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, Ijumaa (27.01.2017) ikiwa ni mkutano rasmi wa kwanza kwa Trump kufanya na kiongozi wa kigeni tangu alipochukua madaraka.

https://p.dw.com/p/2WWaw
Kombi-Bild Donald Trump Theresa May

Baada ya kutoa msimamo wake kuhusu ujenzi wa ukuta mpakani mwa Marekani na Mexico, kuna uwezekano mazungumzo ya Trump na May yakawa mepesi wakati waziri huyo mkuu atakapojaribu kuhathibitisha mahusiano maalum ya Uingereza na Marekani hususan juu ya mustakabali wa nchi hiyo nje ya Umoja wa Ulaya.

Awahutubia wabunge

Theresa May aliwasili  jana nchini Marekani na alikutana na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Paul Ryan na kujadiliana masuala kadhaa ikiwemo juhudi za mwanzo kuhusu mkataba wa kibiashara wakati Uingereza itakapojiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Pia aliwahutubia wabunge wa chama cha Republican mjini Philadelphia na kuwataka kuwa makini na Urusi huku akionya mshirika wake huyo kuongeza jitihada katika usalama wa dunia.

Die britische Premierministerin Theresa May spricht am 26.01.2017 in Philadelphia
Waziri Mkuu Theresa May akiwahutubia wabunge wa MarekaniPicha: Picture-Alliance/dpa/S. Rousseau

Hotuba yake aliyoitoa mbele ya wabunge wa Republlican, May alipongeza ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi hizo mbili. "Wakati wa Uingereza na Marekani kuingilia nchi huru katika jaribio la kuifanya dunia kuwa kama sisi umekwisha. Lakini hatuwezi kumudu kusimama na kukaa kimya wakati kuna kitisho halisi na wakati ni kwa maslahi yetu wenyewe kuingilia kati. Ni lazima kuwa na nguvu,  kuwa na akili na vichwa vigumu. Na ni lazima kuonyesha suluhisho hilo muhimu ili kusimama kwa ajili ya maslahi yetu", alisema May.

May anayo matumaini na mpango wa Marekani kwamba utasaidia kuondoa hofu miongoni mwa wananchi wa Uingereza waliogawanyika kwamba uchumi wa taifa lao unaweza kuwa mbaya baada ya kuonoka katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya. Lakini uamuzi wake wa kukutana na Trump wiki moja baada ya kuapishwa kwake kumeibua sintofahamu nchini Uingereza ambako analaumiwa na wanasiasa wote kwa kauli zake za kibaguzi hii ya wanawake, waislamu na mateso.

Waziri mkuu May ameahidi kuwa "mkweli" katika ushirikiano na bilionea asiyetabirika na kupuuzia maswali ya ikiwa watasikizana. Wawili hao watakutana Ikulu ya Marekani na baadae kufanya mkutano na waandishi wa habari kabla ya chakula cha mchana.

Shada la Maua

Mapema leo May alitembelea makaburi ya taifa ya Arlington, sehemu ambayo askari wengi wa Uingereza waliopigana na vikosi vya Marekani katika vita mbalimbali wamepumzishwa. Kuhusu mvutano unaozidi kupanuka baina ya Marekani na China, kiongozi huyo alisema hofu ya Magharibi kupoteza nguvu haiwezi kutimia ikiwa Uingereza na Marekani zitaendelea kusimama pamoja.

Pia alisema nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO zinapaswa kuchangia kwa usawa, lakini ametetea madai ya Trump kwamba jumuiya hiyo imepitwa na wakati. Pia aliutetea mkataba wa mpango wa nyuklia wa Iran, akisema ulikuwa muhimu sana kwa usalama wa kikanda.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Saumu Yusuf