1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ashikilia msimamo wake vurugu za Charlottesville

Sylvia Mwehozi
16 Agosti 2017

Kwa mara nyingine tena Rais Donald Trump amekariri kauli aliyoitoa awali kwamba makundi yote mawili yenye itikadi kali za mrengo wa kushoto na kulia yalikuwa ya kulaumiwa katika vurugu zilizotokea Charlottesville.

https://p.dw.com/p/2iIzw
New York Präsident Trump
Picha: picture-alliance/AP Images/P.M. Monsivais

Rais huyo kutoka chama cha Republican siku moja kabla alikemea ubaguzi wa rangi na kuyataja makundi ya Ku Klux Klan KKK, na wanazi mambo leo kama "wahalifu na majambazi".

Trump amekabiliwa na ukosoaji kutoka mirengo tofauti ya kisiasa juu ya kauli yake kuhusu vurugu za Virginia siku ya Jumamosi, ambako mkutano wa makundi ya Wanazi Mambo leo na wazungu wanaojiona bora, juu ya kuondolewa kwa sanamu la mwanajeshi wa wakati wa utumwa kulisababisha  kuzuka kwa machafuko dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakipinga ubaguzi wa rangi.

USA Virginia - Ausschreitungen nach Demonstrationen
Waandamanaji wa makundi kibaguzi wakikabiliana na wale wanaopinga ubaguziPicha: Getty Images/C. Somodevilla

Machafuko hayo yaliishia katika umwagaji damu baada ya mtu anayeshukiwa kuwa Mnazi mambo leo James Fields kulivurumisha gari katika umati wa waandamanaji wa kupinga ubaguzi na kumuua mwanamke mmoja na kuwajeruhi wengine 19.

Katika majibizano ya kelele na waandishi wa habari, Trump aliweka wazi kwamba anachoshwa na watu wanaoendelea kuhoji juu ya suala hilo. "Na kulikuwa na kundi upande mmoja lilikuwa baya, na kundi moja upande mwingine lilikuwa na vurugu, na hakuna anayetaka kulisema hili lakini nitalisema hivi sasa. Kulikuwa na kundi lililokuja kuandamana bila ya kibali na kwakweli walitawaliwa na vurugu," alisema Trump katika mkutano na waandishi wa habari.

Maoni ya Trump yalikaribishwa na David Duke, kiongozi wa zamani wa kundi Ku Klux Klan na mtu muhimu katika mkutano wa siku ya jumamosi. Aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema "asante rais Trump kwa ukweli wako na ujasiri wa kusema ukweli kuhusu Charlottesville na kukemea magaidi wa mrengo wa kushoto".

Confederate Monument Protest Charlottesville
Mwanamke mmoja akitembelea sehemu ya kumbukumbu ambako Herther Heyer aliauwa JumamosiPicha: picture-alliance/AP/J. Rendleman

Lakini kwa upande wa mrengo wa kushoto, maneno ya rais Trump yaliibua ghadhabu. Tim Kaine, mgombea wa zamani wa umakamu wa rais kupitia chama cha Democratic na seneta wa kutoka Virginia aliandika kwamba " vurugu za Charlottesville zilichochewa na upande mmoja. Upande wa wazungu wanaojiona bora kueneza ubaguzi wa rangi, kutokuvumiliana na vitisho. Huo ndio ukweli".

Wanachama wenzake na Trump pia nao hawakumung'unya maneno, Spika wa bunge Mrepublican Paul Ryan aliandika kwamba ni "lazima tuwe wakweli. Kundi la wazungu wanaojiona ni bora linachukiza".

Ukosoaji mwingine pia ulitoka nje ya ulingo wa siasa ambapo nyota wa mpira wa kikapu nchini humo LeBron aliandika kwamba"chuki imekuwepo nchini Marekani. Ni kweli tunafahamu lakini Donald Trump amelifanya kuwa fasheni tena".

Baada ya mkutano huo na waandishi wa habari, mkuu wa chama kikuu cha wafanyakazi nchini Marekani cha AFL-CIO aliungana na wakurugenzi wengine kadhaa wa ngazi ya juu kujiuzulu kutoka katika baraza la ushauri wa uzalishaji wa kiviwanda la Donald Trump.

Nje ya jengo la Trump, mamia ya watu waliandamana kupinga ubaguzi lakini walizingirwa na maafisa wa polisi ili kuzuia mapambano na wafuasi wa Trump waliokuwa karibu na eneo hilo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga