Trump kukiunganisha chama cha Republican
5 Mei 2016Jumtano usiku mbunge mwandamizi wa chama cha Repulican katika baraza la seneti Mitch McConell amemuunga mkono rasmi Trump kama mgombea wa chama hicho cha Republican ili kuzuwiya muhula wa tatu wa chama cha Democrat cha Rais Barack Obama anayemaliza muda wake.
McConell amesema Trump ambaye anachukuliwa ndie atayekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho hivi sasa ana fursa na wajibu wa kukiunganisha chama chao katika kutimiza malengo yake.
Ushindi mkubwa wa Trump katika uchaguzi wa mchujo hapo Jumanne katika jimbo la Indiana umewalazimisha wagombea wengine wa chama hicho kubwaga manyanga Ted Cruz na baadae John Kasich gavana wa Ohio ambaye amefanya hivyo hapo jana na kumwachia tajiri huyo bila ya mpizani kuwania tiketi ya kukiwakilisha chama hicho.
Wafuasi wa gavana wa Ohio John Kasich wameelezea masikitiko yao na kuvunjika moyo baada ya kutangaza kwamba anasitisha kampeni yake ya kuwania urais.
Linda Ayish amesema "Nimevunjika moyo kwamba amesitisha kampeni yake.Nimekuwa nikimfahamu gavana Kasich kwa takriban miaka 40. Ni mtu kama vile alivyo katika uhalisia wake. Nafikiri ameendesha kampeni nzuri na nafikiri mwishowe ujumbe wake haukuitikiwa lakini hiyo ndio siasa."
Umoja katika chama
Trump mwenye umri wa miaka 69 amekiambia kituo cha televisheni cha Fox News kwamba sasa watakiunganisha chama na watauwaunganisha watu pamoja.
Lakini kutokana na kutoungwa mkono kwa kiwango kikubwa sana kuwahi kushuhudiwa miongoni mwa wagombea wa urais nchini Marekani wa kipindi cha sasa na wasi wasi ndani ya chama chake chenyewe juu ya tabia yake ya jazba tajiri huyo mara moja ameanza kuchukuwa hatua ya kuondowa wasi wasi juu ya namna atakavyoingoza nchi hiyo.
Ameliambia gazeti la New York Times kwamba anajuwa watu hivi sasa hawana uhakika Rais Trump atakuwa wa aina gani. Amesema lakini mambo yatakuwa mazuri kwamba hagombanii urais ili kuiyumbisha nchi.
Kitendawili cha mgombea mwenza
Trump pia ameanza kutafakari wazo la yule anayeweza kuwa mgombea mwenza wake kwa kukiambia kituo cha televisheni cha ABC News anataka "mtu mwenye uzoefu wa kisiasa" ili kuchanganisha na wake wa kibiashara.
Majina yanayotajwa ni pamoja na seneta Rob Portman wa jimbo la Ohio lenye wapiga kura wengi wasioamuwa chaguo lao na gavana wa jimbo la South Carolina Nikki Haley.
Trump mwenyewe binafsi amesema angeliweza kumfikiria Kasich mbunge wa zamani ambaye amesaidia kuweka uwiano katika bajeti ya serikali kama mgombea mwenza wake.
Kivumbi kikubwa kinachomkabili tajiri huyo kinatoka kwa mgombea wa Demokratik Hilary Clinton mwenye umri wa miaka 68 ambaye anatarajia kuwa Amiri Jeshi wa Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Marekani ambapo kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni yuko mbele ya Trump kwa asilimia 54 dhidi ya 41.
Mwandishi: Mohamed Dahman /AFP/
Mhariri: Josephat Charo