Trump kuamua kuhusu mkataba wa Paris
1 Juni 2017Wahariri pia wamejishughulisha na hali nchini Afghanistan baada ya shambulio la kigaidi ambapo watu zaidi ya 80 waliuwawa jana.
Dunia imelazimika kusubiri kwa siku chache kuweza kufahamu msimamo wa rais wa Marekani Donald Trump, kuhusiana na iwapo atakubali kuwamo ndani ya mkataba huo wa kimataifa ama ataamua vingine. Lakini baada ya kuhudhuria mikutano ya viongozi wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Brussels na ule wa nchi zenye utajiri mkubwa wa viwanda G7 mjini Taormina, Italia, huenda matumaini yakawa yamepotea, na kwamba ni maajabu tu yanaweza kutokea ili kuweza kumfanya rais huyo wa Marekani kuweza kuliangalia suala la mabadiliko ya tabia nchi katika uhalisia wake. Itakuwa hatari sana kwa Marekani kujitoa kutoka mkataba huo, kwa kuwa huo ndio utakuwa mwisho wa ulinzi wa mazingira kimataifa. Vizingiti vingi mno vimeondolewa, tangu mkutano wa Paris, lakini kila mara kunatokea kitu kingine kinakinga.
Gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung likiandika kuhusu mada hiyo ya mkataba wa mazingira, mhariri anaandika, kwamba kujitoa kwa Trump kutoka mkataba wa mazingira ni ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi nchini Marekani. Mhariri anaendelea.
Katika eneo la kati nchini Marekani wananchi wanashangiria akifanya hivyo. Mara chache kauli ya "mimi sijali" inakuwa na maana nzuri. Kile anachoonesha rais huyu wa 45 wa Marekani Donald Trump kuhusu suala hili la mazingira ni kwamba anajaribu kwa njia ngumu sana kujaribu kuleta kitu cha manufaa. Kwa upande wa kisiasa hadi sasa hajaleta chochote cha kujivunia. Lakini ana madaraka kuweza kuvuruga mambo. Mojawapo ya mambo hayo ni kuvuruga msingi wa mabadiliko ya mfumo wa afya ambao umewekwa na mtangulizi wake Barack Obama, ameshambulia kwa ndege za kivita nchini Syria na sasa anataka kuondoa yale yote yaliyopatikana kwa miaka mingi ya majadiliano katika mkataba wa mazingira wa Paris.
Shambulizi la kigaidi Afghanistan
Mada nyingine ni kuhusu shambulio la bomu lililotokea nchini Afghanistan jana ambapo watu zaidi ya 80 waliuwawa. Mhariri wa gazeti la Reutlinger General-Anzeiger anaandika kwamba , kundi la dola la kiislamu IS huenda linataka kuleta mtafaruku miongoni mwa mataifa ya magharibi katika kulishughulikia suala hilo. Mhariri anaendelea kuandika.
Kundi la Taliban limeonesha hivi karibuni kutaka kuzungumza na serikali mjini Kabul huenda ni kutokana na kutambua mbinyo wa ushindani kutoka makundi mengine ya wapiganaji ndani ya nchi hiyo hususan kundi la IS. Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani kwa hilo yuko tayari. Ushahidi ni mfano wa Gulbudidin Hekmatyar. Imewezekana kufanya makubaliano ya amani na mbabe huyu wa zamani wa vita. Hekmatyar sasa sio tena Taliban, lakini wito wake wa kumaliza vita, una uzito mkubwa. Wanapaswa kukaribiana kisiasa. Kupeleka wanajeshi zaidi katika jimbo la Hindukush sio suluhisho.
Mhariri wa gazeti la Nordwest - Zeitung kutoka Oldenburg anaandika kuhusu mada hiyo kwamba wakati mataifa ya magharibi yalipoanza kupunguza majeshi yao nchini Afghanistan vita vilikuwa bado havijamalizika. Mhariri anaendelea.
Ni kama Carl von Clausewitz alivyosema katika karne ya 19 kwamba, Iwapo hutaweza kumshinda, kuna hatari kwamba umeshindwa. Kwa hiyo kuna fursa mbili tu, tuiache Afghanistan ama tuingilie kati kwa kiwango kikubwa zaidi. Kufanya hivyo nusu nusu hakutasaidia.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Josephat Charo