Trump: Hakuna karantini, lakini ushauri kuhusu kusafiri
29 Machi 2020Rais Donald Trump wa Marekani amejizuwia kutangaza karantini kwa ajili ya maeneo hatarishi ya virusi vya Corona mjini New York, New Jersey na Connecticut, badala yake ameelekeza usiku wa Jumamosi kuwa ,taarifa kali ya ushauri kwa wanaotaka kusafiri , itolewe kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo.
Makamu wa Rais Mike Pompeo aliandika katika ukurasa wa Twita kuwa kituo cha udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza CDC anawataka wakaazi wa majimbo hayo matatu , "kujizuwia na safari zisizo za lazima katika muda wa siku 134 zijazo."
Suala la karantini lilipendekezwa na magavana, ikiwa ni Pamoja na gavana wa chama cha Republican Ron DeSantis wa jimbo la Florida, ambe alitaka kuzuwia wasafiri kutoka maeneo yaliyoathirika zaidi kwenda katika majimbo yao.
Lakini hatua hiyo ilikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa viongozi wa majimbo hayo yanayotajwa kuwa na maambukizi makubwa, ambao wameonya kuwa hali hiyo italeta taharuki kubwa katika jamii ambayo tayari imeathirika kwa virusi.
Trump alitangaza kuwa amefikia uamuzi huo baada ya mashauriano na kikosi kazi cha Ikulu ya White house kinachoongoza hatua zinazochukuliwa na serikali kuu na magavana wa majimbo hayo matatu. Amesema amekiagiza kituo cha udhibiti na kuzuwia magonjwa , CDC , kutoa ushauri mkali wa kusafiri, utakaotekelezwa na magavana, kwa kushauriani na serikali kuu. Ameongeza kuwa karantini haitakuwa lazima.
Athari katika sekta za maisha ya jamii
Zaidi ya theluthi moja ya watu wote duniani wamefungiwa hawatoki nje wakati virusi vinasababisha athari kubwa katika karibu kila sekta ya maisha ya jamii, vikifuta mamlioni ya ajira, mbinyo katika huduma za afya na kuleta shinikizo kubwa katika hazina za taifa kwa miaka mingi ijayo.
Duniani , idadi ya vifo imepita 30,000 na maafisa katika baadhi ya nchi wanasema hali mbaya zaidi bado inakuja.
Lakini katika mji wa Wuhan nchini China, ambako virusi hivyo vilijitokeza kwa mara ya kwanza , maafisa wamechukua hatua za awali kuelekea katika hali ya kawaida, kwa kufungua sehemu ya mji huo baada ya zaidi ya miezi miwili kuutenga kabisa mji huo wenye wakazi wapatao milioni 11. Ukilinganisha na Marekani, Mataifa ya Ulaya yameathirika zaidi kwa msingi wa uwiano wa watu, ambapo vifo 20,059 vimetokea.
Italia yazidi kuathirika na virusi vya corona
Italia siku ya Jumamosi ilitangaza vifo vipya 889, na kufikisha zaidi ya vifo 10,000. Uhispania , ambayo ina idadi ya pili ya juu ya vifo kutokana na virusi vya corona, iliongeza vifo 832 katika jumla ya vifo 5,812. Madrid imeimarisha hatua ya kuzuwia watu kutoka nje , na kuzuwia shughuli zote ambazo si za lazima, licha ya kuwa maafisa wamesema janga hilo nchini humo linaonekana kufikia kilele chake.
Urusi ambayo imeripoti viwango vya chini vya maambukizi, imesema itafunga mipaka yake Jumatatu katika juhudi za kupunguza kusambaa kwa virusi. Zaidi ya mambukizi 640,770 ya virusi vya Corona yamerekodiwa rasmi duniani kote tangu kuzuka kwa virusi hivyo mwishoni mwa mwaka jana, kwa mujibu wa idadi iliyotolewa na shirika la habari la Ufaransa AFP.
Nchini Ufaransa, ambayo imeshuhudia vifo karibu 2,000, waziri mkuu Edouard Philippe amenya kuwa mapambano ndio kwanza yanaanza. Wiki mbili za kwanza za mwezi Aprili zitakuwa ngumu zaidi kuliko wiki mbili zilizopita, amesema.
Uingereza imefikisha watu 1,000 waliofariki kutokana na ugonjwa huo COVID-19.