Trump: EU ondoeni vizuwizi tutaondoa ushuru
11 Machi 2018Rais wa Marekani amesema hayo baada ya mazungumzo magumu mjini Brussels kati ya wajumbe wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya na mwakilishi wa masuala ya biashara wa Marekani Robert Lighthizer katika juhudi za kumaliza mzozo mkubwa ambao wengi wanahofia unaweza kuingia katika vita vikubwa vya kibiashara.
Afisa wa ngazi ya juu wa biashara wa Umoja wa Ulaya amesema Marekani imeshindwa kueleza kwa uwazi juu ya vipi Ulaya na Japan zinaweza kuepuka kodi hizo zinazotarajiwa kuanza wiki ijayo.
"Umoja wa Ulaya , mataifa safi kabisa ambayo yanaitendea Marekani vibaya kabisa katika biashara, yanalalamika juu ya kodi katika chuma cha pua na bati," Trump alisema.
"Iwapo wataondoa vizuwizi vyao vibaya kabisa na kodi katika biadhaa za Marekani zinazotozwa hivi sasa, tutafanya hivyo hivyo kuondoa vyetu. Nakisi kubwa. Iwapo hawatafanya hivyo, tutaweka kodi kwa magari. Haki!"
Tangazo la rais Donald Trump la kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa chuma cha pua kitakachoingizwa nchini humo na asilimia 10 katika madini ya bati limeuchoma Umoja wa Ulaya, pamoja na washirika wengine wakubwa ikiwa ni pamoja na Japan, ambayo waziri wake wa uchumi Hiroshige Seko pia alihudhuria mazungumzo hayo mjini Brussels.
Matarajio ya EU
"Kama washirika wakubwa wa usalama wa Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan wamemsisitizia balozi Lighthizer matarajio yao kwamba mauzo ya nje ya Umoja wa Ulaya na Japan kwenda Marekani yataondolewa katika kutozwa ushuru huo mkubwa," taarifa ya Umoja wa Ulaya imesema baada ya mazungumzo hayo.
Lakini baada ya mazungumzo ya pande mbili na Lighthizer, kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Cecilia Malmstroem aliandika katika ukurasa wa Twitter: "Hakuna maelezo ya wazi juu ya utaratibu hasa wa Marekani wa msamaha wa ushuru hata hivyo, kwa hiyo majadiliano yataendelea wiki ijayo."
Umoja wa Ulaya umekwenda umbali zaidi katika mapambano dhidi ya hatua hizo za kushitua za Marekani, kwa kutangaza orodha ya bidhaa za Marekani zitakazoathirika na hatua za kulipiza kisasi iwapo bidhaa zake zitaathirika na ushuru huo. Katika kutangaza hatua hizo, rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker alimshambulia Trump, akisema Umoja wa Ulaya unaweza kupambana na "ujinga kwa ujinga."
Lighthizer, mfuasi mtiifu kwa kauli mbiu ya Trump ya "Marekani kwanza" hakutoa tamko rasmi baada ya mazungumzo hayo, lakini pande hizo tatu zilikubaliana kuhusu hatua kadhaa za kupambana na uwepo wa bidhaa nyingi katika soko duniani kote za chuma cha pua na nyingine, hususan kutoka China.
Hatua hizi "hazikutarajiwa" na ni chanzo cha matumaini ya tahadhari kuhusu kutatuliwa kwa mzozo huu wa ushuru, amesema afisa wa Umoja wa Ulaya kwa masharti ya kutotajwa jina.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Jacob Safari Bomani